Wadau wa kahawa watakiwa kutumia fursa ya masoko

Muktasari:

Wadau wa kahawa wametakiwa kutumia fursa ya masoko ya ndani na nje ya nchi ili kupata tija inayotokana na zao hilo. 

Mbozi. Wadau wa kahawa wametakiwa kutumia fursa ya masoko ya ndani na nje ya nchi ili kupata tija inayotokana na zao hilo.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Anna Joram Kidalya akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Waziri Kindamba katika maadhimisho ya Siku ya Kahawa Duniani yaliyofanyika kikanda katika Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe Jumamosi Oktoba 1, 2022.

Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa kahawa imekuwa ni kinywaji kinachotumiwa sana duniani baada ya maji hivyo inajidhirisha kutoka takwimu za kimataifa kutoka Shirika la Kahawa Duniani la ‘International Cofee Organization’ kuwa kila siku vikombe bilioni 2.7 hunywewa na wanyaji wa kahawa.


Katika maadhimisho hayo yenye kaulimbiu ya Kahawa kuwa Ajenda ya 10/30 kilimo cha kahawa chenye ubora kuzingatia tabia ya nchi ili kuongeza tija, Kidalya alisemakuwa lengo la kaulimbiu hiyo ni kukumbusha wadau kuwa maendeleo ya sekta ya kahawa yanategemea sana ushiriki katika kutunza mazingira kwa kutumia mbinu mbalimbali kukabiliana na tabia ya nchi ikiendana na maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Kilimo kuwa kilimo ni biashara.

Aliongeza kuwa ili kahawa iwe na bei nzuri na iliyobora ni lazima kuzingatie masharti ya kuandaa kahawa.

Pia, ametoarai kwa wadau kuhamasisha unyaji wa kahawa huku akieleza kuwa dhana ya kinywaji hicho kuwa na madhara kiafya sio kweli.

“Ili kuepukana na kutegemea soko la nje tuendelee kuhamasishana kuhusu faida nyingi zitokanazo na kahawa na kuondoa dhana iliyojengeka miongoni mwa jamii kuwa kinywaji hiki kina madhara kwa afya jambo ambalo si sahihi.’’ amesema

Awali, akisoma risala katika maadhimisho hayo, Meneja wa Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (TaCRI) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Dismas Pangalas alisema kuwa wadau mbalimbali walipata fursa ya kukutana pamoja kuhamasishana kunywa kahawa kwa pamoja.

Pangalas amesema kuwa unywaji wa kahawa ni mdogo sana ambao kwa wastani ni asilimia saba.

Aliongeza kuwa kupitia maadhimisho hayo wadau mbalimbali wa kahawa ikiwemo wakulima wadogo na wakubwa walipata fursa ya kukutana na viongozi mbalimbali wa Serikali, wataalamu, watafiti, wasindikaji, wanunuzi wadogo na wakubwa, taasisi za kifedha na wauzaji wa pembejeo za kahawa.

“Katika jukwaa hili pia wadau walipata wasaa wa kujadili mafanikio na changamoto wanazokutana nazo na utatuzi wake” alisema Pangalas

Hata hivyo zao la kahawa limekuwa ni miongoni mwa mazao ya kimkakati ambayo yamekuwa yakipewa kipaumbele katika mpango wa maendeleo.

Vilevile zao la kahawa lina fursa kubwa za kuchangia katika kufikia malengo ya maendeleo katika taifa kama ilivyo ainishwa katika agenda 20/30 ambapo zao la kahawa limechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha maisha ya mkulima na kuongeza kipato cha kaya.