Wadau wa utalii watakiwa kushiriki tamasha la utamaduni Moshi

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Steven Kagaigai akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo kuhusu tamasha la utamaduni ambalo litahudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan Januari 22, 2022. Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai amewataka wadau wa  kampuni za utalii mkoani humo pamoja na wananchi  kujitokeza na kushiriki katika  tamasha la utamaduni litakalo hudhuriwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan Januari 22, 2022.

Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai amewataka wadau wa  kampuni za utalii mkoani humo pamoja na wananchi  kujitokeza na kushiriki katika  tamasha la utamaduni litakalo hudhuriwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan Januari 22, 2022.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Januari 18, 2022 amesema kuhudhuria kwao katika tamasha hilo watapata fursa ya kutangaza utamaduni kama bidhaa kwa wateja wao na kulitangaza tamasha hilo ambalo litaendelea kuwa endelevu katika mkoa wa Kilimanjaro.

Kagaigai amesema kwenye tamasha hilo ambalo litafanyika katika viwanja vya Ushirika vilivyopo Manispaa ya Moshi kutakuwa na maonyesho ya vyakula vya asili, historia ya Himaya za kichifu na burudani kwa baadhi ya makabila yaliyopo katika mkoa huo hususani wachaga, wapare na wamasai.

"Uongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro kwa kushirikiana na umoja wa machifu pamoja na wizara ya utamaduni sanaa na michezo, tumeandaa tamasha la utamaduni mkoani hapa ambalo litafanyika Januari 22 mwaka huu"amesema Kagaigai

"Tamasha hili ni fursa kwa sekta nyingine ikiwamo sekta ya utalii, ubunifu, afya hususani tasnia ya lishe na sekta nyingine nyingi zitanufaika na tamasha hili, nawakaribisha wadau kama vile kampuni za utalii na wengineo waje wauze utamaduni wetu kama bidhaa kwa wateja wao,"

Amewataka wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kuungana na Rais katika siku hiyo adhimu katika viwanja vya chuo kikuu cha Ushirika