Wadau wagawanyika ukomo vitambulisho vya Nida

Muktasari:

  • Serikali kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni imetangaza mpango wa kufanya mabadiliko ya kanuni ya utambuzi na usajili kuondoa ukomo wa matumizi wa vitambulisho vya Taifa (Nida).

Mwanza. Mpango wa Serikali wa kuondoa ukomo wa muda wa vitambulisho vya Taifa unaonekana kuwagawa wadau kwa baadhi kuunga mkono huku wengine wakipinga.

 Wakitoa maoni yao leo Jumatano Februari 22, 2023 wakati wa mjadala ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited kupitia mtandao wa kijamii ya Twitter ya Mwananchi Twitter Space, wadau hao kila upande umetaja sababu za ama kuunga mkono au kupinga mpango huo.

Akichokoza mada inayosema “Vitambulisho vya Taifa kuondolewa ukomo kuna athari gani?” mmoja wa wachokoza mada, William Shao amesema uamuzi huo una faida chanya na hasi kwa wananchi na Serikali yenyewe.

“Faida ya kuhuisha kitambulisho mara kwa mara ni kutoa fursa ya kuingiza taarifa mpya kulingana na anuani ya makazi, umri, picha na mabadiliko ya teknolojia,” amesema Shao

Faida nyingine kwa mujibu wa Shao ni kuondolewa kwenye orodha watu wanaofariki dunia na wale ambao pengine walipata vitambulisho vya Taifa bila kuwa na uhalali.

“Tunapotoa vitambulisho vya Taifa visivyo na ukomo ni lazima tuwe na umadhubuti kufahamu iwapo wanaovipata kweli ni uraia wa Tanzania,” amesema

Huku akitaja baadhi ya Mataifa ikiwemo Kenya, Batswana na Ghana vyenye utaratibu wa vitambulisho vya Taifa visivyohuishwa, mchokoza mada huyo amesema kutohuisha vitambulisho kunaweza kusababisha mabadiliko muhimu ya taarifa kukosekana.“Kuna umuhimu wa kubadilisha vitambulisho vya Taifa kuwezesha kuingizwa kwa taarifa mpya ikiwemo picha, anwani ya makaazi, umri na vitu vingine vingi. Tunaweza kupanga labda muda wa miaka mitano au 10 kuhuisha vitambulisho hivyo,” amesema Shao

Hoja ya kuisha vitambvulisho iliungwa mkono na mzungumza mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Abdallah Suleiman aliyezungumza kutokea nchini Ubelgiji akisema utawezesha kuingizwa kwa taarifa mpya huku akishauri uwekwe muda wa mika 10 wa kuhuisha vitambulisho.

“Serikali pia itumie mabadiliko ya vitambulisho kama sehemu ya kipato kwa kutoza gharama ya kupata vitambulisho vipya kama inavyofanyika kwenye hati za kusafiria,” amesema Suleiman

Ili kuondoa usumbufu wa misururu mirefu wakati wa kubadilisha vitambulisho kama ilivyoshuhudiwa wakati uliopita, mchangiaji huyo alishauri utoaji ufanyike kwa awamu kutoka mkoa mmoja hadi mwingine kuhakikisha vitendea kazi na watumishi wanakuwa eneo moja kabla ya kuhamia eneo nyingine.

Mzungumzaji mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Paul James yeye ameunga mkono mpango wa Serikali wa kuondoa ukomo wa muda wa vitambulisho vya Taifa akisema itaondoa usumbufu kwa wananchi kuanza kutafuta vitambulisho vipya.

“Muhimu ni kuweka mfumo maalum wa kupata na kuingiza taarifa mpya za mabadiliko ikiwemo umri, anwani, picha na hata taarifa za vifo,” amesema James

Mzungumzaji aliyejitambulisha kwa jina la Mndeme Sultan, alisisitiza umuhimu wa kuhuisha vitambulisho kuwezesha taarifa za wanaobadilisha ama dini au uraia kuingizwa kwenye vitambulisho.