Wadau wamshukia Mbunge Ngara, wadai ni joto la uchaguzi

Mbunge wa Ngara, Ndaisaba Ruhoro

Dar es Salaam. Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamekosoa vitendo vya mbunge anayetuhumiwa kulazimisha wananchi kuweka picha yake kwenye maeneo yao ya kazi na nyumbani.

Wamevihusisha vitendo hivyo na homa ya uchaguzi ujao wa mwaka 2025, huku wakieleza anachokifanya hakiwezi kumsaidia.

Hivi karibuni katika mitandao ya kijamii zilisambaa taarifa za wananchi waliodai wanalazimishwa na mbunge wa Ngara, Ndaisaba Ruhoro (CCM), kuweka picha zake katika maeneo yao.

Hata hivyo, mbunge huyo alisema picha hizo ni kwa ajili ya ndugu zake na wananchi wengine wanafanya hivyo kwa mapenzi yao kwake.

Ruhoro alizindua kampeni ya kusambaza picha zenye sura yake, kalenda na vipeperushi kwa ajili ya ndugu, jamaa, marafiki na familia, akifafanua kuwa picha yake itapatikana ikiwa kwenye fremu zenye rangi tofauti. “Ninazindua rasmi kampeni ya kusambaza picha, kalenda na vipeperushi vyenye sura ya mbunge wenu, mbunge wa Ngara mimi mwenyewe Ndaisaba George Ruhoro,” alisema.

Alisema alipokuwa akiomba kuchaguliwa na wapiga kura alitumia picha, ndiyo maana watu walimuona na kumchagua, hivyo wananchi hawana budi kujiamini kuweka picha hiyo wanapotaka bila kuogopa na wanaokataa wana nongwa.

Mbali na hilo, Novemba mwaka 2021 mbunge huyo aliibua mjadala akituhumiwa kuwanyanyasa vijana waliotunga wimbo wa kumkumbusha kutekeleza ahadi zake.

Ruhoro alikana tuhuma hizo, akisema ameupenda wimbo huo kwa kuwa unawakumbusha viongozi kutimiza wajibu.


Wachambuzi wakosoa

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dodoma (Udom), Paul Loisulie alisema anachofanya mbunge huyo ni ulimbukeni, kwa sababu picha hazina umuhimu wowote kwa wananchi. “Tunaweza kusema ni ulimbukeni maana picha hazina msaada wowote,” alisema.
Alisema mbunge anatakiwa kutekeleza ilani ya chama na ahadi alizotoa kwa wananchi ili waendelee kumkumbuka.

Loisulie alisema kama kuna wanaotetea kampeni ya kusambaza picha watakuwa na masilahi binafsi, kwa kuwa anaamini wanafahamu picha hazina umuhimu kwa wananchi. “Huenda hadharani wako sawa, lakini ndani watakuwa wanaonyana,” alisema.

Akizungumzia kampeni hiyo, alisema huenda ni homa ya uchaguzi ujao, lakini atambue kuwa picha zitasaidia kufahamika ila hazitatatua hoja.

Kwa upande wa Mhadhiri wa Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda aliunga mkono hoja ya Dk Loisulie, akisema wabunge wengi wa awamu iliyopita kwa namna walivyoingia madarakani huenda wameanza kampeni kwa uchaguzi ujao.

Dk Mbunda alisema huenda mbunge huyo anahisi hafahamiki jimboni kwake na anafanya hivyo kama njia ya kujitangaza kwa wananchi. Alisema wapo wabunge wanaogawa cherehani na baiskeli kwa wananchi majimboni, lakini kugawa picha haoni kama ni kampeni.

Akilifafanua hilo, Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ngara, John Mapange alisema mbunge huyo amefanya kazi kubwa jimboni, jambo linalowafanya wananchi wampende.

“Wananchi wamechukua picha hizi kwa mapenzi yao na ofisi ya mbunge imekuwa ikizitoa kwa kadiri wananchi wanavyohitaji na hakuna mwananchi aliyepewa kwa lazima,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ngara, Vitalis Ndailagije alisema picha zinazosambaa kwa wananchi hazijagharimiwa na mbunge.
Hata hivyo, mfanyabiashara wilayani Ngara ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema picha aliyoiweka eneo lake la biashara hakuinunua, alipewa na wapambe wa mbunge huyo.