Prime
Wadau waonya kuporomoka ‘GS’ matokeo kidato cha sita
Muktasari:
- Wabainisha kuwa, kushuka kwa ufaulu wa somo hilo ni ishara inayohitaji hatua za haraka ili kuhakikisha wanafunzi hawapati elimu inayowaandaa kwa mitihani pekee, bali elimu inayowajenga kuwa viongozi na wananchi wenye uelewa mpana wa jamii yao
Dar es Salaam. Wakati matokeo ya mtihani wa Kidato cha Sita mwaka 2026 yakionesha ufaulu kupanda, wadau wa elimu wameeleza wasiwasi kuhusu mwenendo wa ufaulu wa Somo la Maarifa ya Jumla (General Studies-GS).
Wamesema kushuka kwa kiwango cha ufaulu kunaweza kuathiri uwezo wa wanafunzi kuwa raia wenye uelewa mpana wa masuala yanayoizunguka jamii.
Wadau hao wamebainisha kuwa kushuka kwa ufaulu wa somo hilo ni ishara inayohitaji hatua za haraka ili kuhakikisha wanafunzi hawapati elimu inayowaandaa kwa mitihani pekee, bali elimu inayowajenga kuwa viongozi na wananchi wenye uelewa mpana wa jamii yao.
Takwimu za matokeo ya mtihani huo zinaonesha kuwa kati ya wanafunzi 125,149 waliofanya mtihani wa somo hilo, takribani asilimia 4.33, sawa na wanafunzi 5,419, walipata daraja la F, hali ambayo imeibua mjadala kuhusu sababu zinazochangia wanafunzi kutofanya vizuri katika somo hilo.
Matokeo hayo yanaonesha kuwa asilimia 95.67 ya wanafunzi walipata madaraja ya A hadi S, huku wengi wao wakiwa katika madaraja ya D, E na S.
Kwa mujibu wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) asilimia 0.00 wamepata daraja A, asilimia 0.37 daraja A hadi B, asilimia 6.61 wamepata daraja A hadi C, asilimia 38.80 wamepata A hadi D na asilimia 85.03 wamepata daraja A hadi E.
Ufaulu katika somo hilo umeshuka kwa asilimia 0.99 ikilinganishwa na matokeo ya mtihani wa mwaka 2024 ambapo asilimia 96.66 ya wanafunzi walipata daraja A hadi S, asilimia 3.34 sawa na wanafunzi 4203 walipata daraja F.
Akizungumzia hilo, jana Julai 7, 2026, Katibu Mtendaji wa Necta, Profesa Said Mohamed amesema hali hiyo imechangiwa na wanafunzi kuweka mkazo kwenye masomo ya tahasusi na kulipa kisogo somo hilo.
“Tumeona ufaulu wa hili somo huko chini kwa sababu wanafunzi wanaliona ni somo la jumla wakati wao nguvu yao wameweka kwenye masomo ya tahasusi, sasa kwa sababu kuna haya mabadiliko ya mtaala tukiona haliendelewi kupewa uzito, tutaliweka kikanuni katika mfumo wa grading kama njia ya kuliimarisha zaidi,” amesema.
“Nitoe wito kwa wadau wakiwemo wazazi, walimu hata wanafunzi wenyewe watambua kuwe hilo somo limewekwa kimkakati pamoja na kujua Kemia na Fizikia ni muhimu pia kujua mambo mengine mtambuka” amesema Profesa Mohamed.
Mitizamo ya wadau
Kufuatia hilo Mwananchi imezungumza na wadau wa elimu ambao wameeleza General Studies ni somo lenye nafasi muhimu katika kuwaandaa wanafunzi kuelewa masuala mbalimbali ya kijamii, kiuchumi, kisiasa, mazingira, sayansi na teknolojia, hivyo kushuka kwa ufaulu wake kunapaswa kuchukuliwa kwa uzito.
Wadau hao wamependekeza kuimarishwa kwa mbinu za ufundishaji wa somo hilo, ikiwamo kutumia mifano halisi ya matukio yanayotokea nchini na duniani ili kuwafanya wanafunzi walione lina uhusiano wa moja kwa moja na maisha yao.
Kwa mujibu wa wadau hao, General Studies inapaswa kuendelea kupewa nafasi inayostahili kwa kuwa, inachangia kujenga kizazi chenye uwezo wa kuchanganua changamoto za Taifa, kuelewa haki na wajibu wao, pamoja na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa maendeleo ya Tanzania.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Leonard Ngabo amesema changamoto ya somo hilo inaweza kuwa inatokana na namna linavyofundishwa na kutafsiriwa na wanafunzi wengi kama somo lisilo na uzito mkubwa ukilinganisha na masomo mengine yanayohusiana moja kwa moja na taaluma wanazokusudia kusoma vyuo vikuu.
“General Studies si somo la kukariri kwa ajili ya mtihani pekee, bali linamlenga mwanafunzi kuwa na uwezo wa kuchambua mambo yanayotokea katika jamii yake. Linawajengea uwezo wa kufikiri kwa kina, kufanya maamuzi na kushiriki katika maendeleo ya nchi,” amesema.
Amesema katika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo mabadiliko ya tabianchi, maendeleo ya teknolojia, mabadiliko ya kiuchumi na masuala ya utawala bora, vijana wanahitaji maarifa mapana yanayotolewa kupitia somo hilo.
Daniel Mwasi ambaye ni mwalimu wa shule ya sekondari amesema baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakilipa uzito mdogo somo hilo kwa sababu halionekani kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na taaluma wanazotaka kusomea.
Amesema mtazamo huo umechangia wanafunzi kutotenga muda wa kutosha kulisoma, hali inayosababisha kushuka kwa ufaulu.
“Wanafunzi wengi huwekeza nguvu zaidi kwenye masomo wanayoamini yatawasaidia kupata nafasi za vyuo vikuu. Ingekuwa kama vile zamani ukifeli GS inakushushia pointi kwenye tahasusi yako nafiki wangeliwekea nguvu zaidi tofauti na ilivyo sasa.
“Ukweli ni kwamba General Studies ina mchango mkubwa katika maisha yao ya kila siku kwa sababu linawafundisha namna ya kuelewa jamii na mazingira yanayowazunguka,” amesema Mwasi.
Baadhi ya wazazi wameitaka Serikali kupitia Wizara ya Elimu na wadau wengine kuangalia upya namna ya kuongeza hamasa kwa wanafunzi kuhusu umuhimu wa somo hilo.
Mkazi wa Mtoji Kijichi, Fransica Ngonyani ambaye pia ni mzazi amesema elimu haipaswi kulenga kumpa mwanafunzi alama pekee, bali inapaswa kumjenga kuwa mtu mwenye uwezo wa kutambua wajibu wake katika jamii.
“Tunapaswa kuwasaidia watoto wetu kuelewa kuwa elimu wanayoipata darasani inapaswa kuwafanya wawe raia bora. General Studies inafundisha mambo ambayo kila Mtanzania anayehusika na maisha ya jamii anapaswa kuyafahamu,” amesema.a