Wadau wapendekeza mambo 10 marekebisho Sera ya Mambo ya nje

Mkurugenzi wa Utafiti, Ubunifu na Ushirikishwaji wa Jamii kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (Saut) Mwanza, Dk Delphine Kessy akizungumza kwenye kongamano la kukusanya maoni ya wadau kuhusu marekebisho ya Sera mpya ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 iliyofanyika jijini Mwanza. Picha na Anania Kajuni

Muktasari:

  •  Kukibidhaisha Kiswahili, ushiriki wa diaspora, mila na desturi, uchumi wa buluu, jinsia na vijana, na sayansi na teknolojia ni miongoni mwa maoni yaliyotolewa na wadau kwenye marekebisho katika Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 ili kuleta tija zaidi.

Mwanza. Wadau mbalimbali mkoani Mwanza wametaja mapendekezo 10 ya kufanyiwa marekebisho kwenye Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 ili kuleta tija zaidi.

Wakizungumza leo Aprili 19, 2024 kwenye kongamano la kukusanya maoni kuhusu sera hiyo mkoani humo, wametaja wamependekeza hayo kuwa ni kukibidhaisha lugha ya Kiswahili, ushiriki wa diaspora, mila na desturi, uchumi wa buluu, jinsia na vijana, na sayansi na teknolojia.

Mambo mengine ni kuwepo kwa utaratibu maalumu wa kupata mabalozi, uraia pacha, uchumi wa kidiplomasia na vazi maalumu la Taifa.

Akizungumza kwenye kongamano hilo, katibu wa ACT Wazalendo Mkoa wa Mwanza, Butije Hamisi ameomba sera itambue uraia pacha ili kutoa nafasi ya raia wenye asili ya Tanzania kuwa na uraia, lakini pia ameomba sera ianishe maeneo ya wawekezaji wa nje kuja kuwekeza nchini.

“Napendekeza sera yetu itambue uraia pacha kwa sababu kuna wenzetu wana asili ya Tanzania, wako katika mataifa mengine wamelazimika kubadilisha uraia ili waweze kunufaika na fursa za huko sasa wanashindwa kunufaika na baadhi ya fursa nchini.

“Taifa letu kwa sasa linahamasisha uwekezaji na tunataka watu kutoka nje wawekeze nchini, lakini mara nyingi tumebaki wafanyakazi wa kampuni kubwa kutoka nje ya nchi, sasa sera yetu iweke wazi maeneo gani watu wanapaswa kuja kuwekeza na ijikite kwa wale wanaokuja kuwekeza wazalishe bidhaa itakayouzwa nje ya nchi, sio kuendelea kuwa wazalishaji wa malighafi,” amesema Hamisi.

Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Chadema, Khalid Seleman akichangia kuhusu jinsia na vijana ameomba sera hiyo kuzingatia uundwaji wa baraza la vijana nchini litakaloweza kushindana na vijana kutoka nje ya nchi.

“Nendeni mkatengeneze Baraza la Vijana la Kitaifa, msiogope, jifunzeni kupitia Rwanda wametengeneza linaitwa 'Youth Connect Rwanda' sasa vijana wao wanaenda kutengeneza mazingira mazuri mpaka kufika 2030 wanaenda kuwa hub ya teknolojia kwa sababu wamefungua dawati la vijana kujadiliana je, sisi tunashindwaje?” amesema.

Seleman akizungumzia kuhusu upatikanaji wa mabalozi, ameiomba wizara hiyo kuweka vigezo maalumu vya kuwapata wawakilishi hao na sio kwa njia ya uteuzi, lakini pia amegusia suala la teknolojia kuwa linahitaji kupewa kipaumbele katika sera hiyo.

Mkurugenzi wa Utafiti, Ubunifu na Ushirikishwaji wa Jamii kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino (Saut) Mwanza, Dk Delphine Kessy amependekeza sera ya uchumi wa buluu ipewe kipaumbele zaidi ikiwa ni pamoja na kulinda maziwa na bahari, lakini pia amependekeza lugha ya Kiswahili ipewe thamani ili kujenga taswira ya Tanzania.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa ametaja sababu nne za kufanya maboresho hayo ni kupata maoni ya kurekebisha sera ya mwaka 2001, kutekeleza agizo la Rais, Samia Suluhu Hassan la kukusanya maoni kwa wananchi kuhusu sera hiyo, kutengeneza sera itakayoitambulisha nchi kimataifa lakini pia ili kuboresha diplomasia ya uchumi.

Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Mbarouk Nassor ambaye pia alikuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo, amesema baada ya kubaini mapungufu yaliyopo katika sera hiyo wanafanya maboresho hayo, ili kuleta tija na kuendana na mazingira ya sasa na baadaye.

"Hii ni fursa kwenu pekee kushiriki katika mchakato wa kuboresha sera ikizingatiwa imepita miaka 23 toka ianze kutumika. Hivyo  ni fursa kwa kizazi hiki kuboresha sera hii ambayo itaongoza Taifa letu kwa miaka mingi baadaye," amesema Balozi Mbarouk.