Wadau wapongeza mkakati wa MCL wa Farm Clinic

Mdau wa kilimo Mkurugenzi wa Shamba fm, Fredy Herbet akizungumza wakati wa kongamano la kilimo jinini Mbeya

Muktasari:

Wadau wa vyombo vya habari nchini wamesema mkakati wa Mwananchi Communications Ltd (MCL) wa Farm Clinic unapaswa kuungwa mkono kwa sababu unalenga kusukuma ajenda ya 10/30 kwenye sekta ya kilimo.

Mbeya. Wadau wa vyombo vya habari nchini wamesema mkakati wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) wa Farm Clinic unapaswa kuungwa mkono kwa sababu unalenga kusukuma ajenda ya 10/30 kwenye sekta ya kilimo.

 Juzi Jumatano, Agosti 3, 2022 Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa alizindua ushirikiano wa MCL, Vodacom na Wizara ya Kilimo kwenye farm Clinic inayolenga kusukuma ajenda ya 10/30.

Wakizungumza katika Kongamano la Shamba Darasa lililoandaliwa na MCL kupitia Farm Clinic katika ukumbi wa Tari Jijini Mbeya yanakofanyika maadhimisho ya Wakulima ya Nanenane, wadau hao wamesema mkakati huo njia inayoonyesha wajibu wa vyombo vya habari kwenye sekta ya kilimo.

Mkurugenzi wa Shamba fm, Fredy Herbet alisema vyombo vya habari vinao mchango mkukwa katika kuhakikisha ajenda ya 10/30 inafanikiwa.

 “MCL wamefikiria jambo kubwa kuanzisha Farm Clinic nadhani sisi kama sekta ya habari tunatakiwa kuwaunga mkono Mwananchi kwa sababu wote tunatakiwa kusukuma ajenda ya 10/30 ifanikiwe haraka,” alisema.

Mwandishi wa Gazeti la Nipashe, Martha Sambo alisema ipo haja ya kuwepo wanahabari waliobobea kwenye masuala ya kilimo ili kusukuma ajenda hiyo.

“Sio mbaya kuwa na maafisa ugani wanahabari ambao wanapoandika, wataandika mahitaji ya msingi ya wakulima kuifikia ajenda hiyo. Sisi kama wanahabari tupo tayari kushiriki katika kuhakikisha wakulima wanafanikiwa kuingia kwenye kilimo biashara kama ilivyo malengo ya ajenda hiyo,” alisema Sambo.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kilimo Tanzania (TARI), Dk Godfrey Lukamilo alisema kwenye utendaji wao wa kazi vyombo vya habari vimekuwa vikitumika kama njia ya kufikisha elimu na teknolojia zinazovumbuliwa kwa wakulima.

“Suala la kufikisha teknolojia linahitaji wadau wengi, tunathamini sana mchango wa wanahabari katika kuifikisha teknolojia tunayovumbua kwa wakulima,” alisema Dk Lukamilo.