Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wadau wasisitiza elimu matumizi nishati safi

Meneja wa mradi wa CookFund  Imanuel Muro akiongea na wadau katika mjadala wa nishati safi jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Elimu imetakiwa kutolewa kwa wananchi ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Dar es Salaam. Ili kupunguza athari za uharibifu wa mazingira, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mitaji na Uwekezaji (UNCDF), limesisitiza umuhimu wa kutolewa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa jamii.

Wito wa shirika hilo, unakuja wakati Afrika inaongoza kwa uzalishaji wa kuni kwa asilimia 37 na mkaa kwa asilimia 66 na kusababisha athari za kimazingira na kiafya.

Hayo yameelezwa na Meneja wa mradi wa CookFund wa UNCDF, Imanuel Muro katika warsha iliyoandaliwa na shirika hilo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kutoa fursa kwa wadau kujadili matumizi ya nishati safi.

Amesema shirika hilo tayari limetangaza mpango wa kitaifa wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi, ukilenga kufanikisha azma ya Serikali kufikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi mwaka 2034.

Ameeleza zitatumika kampeni zinazowahusisha watu mashuhuri kuhakikisha hamasa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia inaongezeka kwa wananchi.

“Matumizi makubwa ya mkaa yanaathiri misitu na kusababisha mabadiliko ya tabianchi, hivyo juhudi za pamoja zinahitajika kuhakikisha upatikanaji wa teknolojia nafuu na bora,” amesema.

Kwa mujibu wa Muro, asilimia 67 ya kaya za mjini, zinamiliki angalau kifaa kimoja cha nishati safi, lakini changamoto za gharama na uelewa ni kubwa.

“Ili kuimarisha matumizi ya nishati safi, wadau wamependekeza kuimarisha usambazaji wa teknolojia kama PayGo LPG na majiko bora, kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vyenye viwango, na kupanua wigo wa programu kufikia maeneo mapya,” amesema.

Akiwasilisha utafiti wake katika warsha hiyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Innocent Pantaleo amesema matumizi ya mkaa yana madhara kiafya na kimazingira.

Amesema inapotumika nishati safi ni muhimu kwa kuhifadhi mazingira na kuboresha afya, hasa za wanawake ambao hutumia muda mwingi jikoni.