Wafanyabiashara 52 Kariakoo wamburuza mmiliki wa jengo baraza la ardhi

Jengo la ghorofa moja linalomilikiwa na kampuni ya Phinison Investment  Limited, lililopo mtaa wa Mchikichi, Kariakoo, Plot namba 4, Block 18, ambalo wapangaji 52  waliopanga wamedai  kutaka kuondolewa kinyume cha utaratibu kabla ya mkataba kuisha.

Muktasari:

  • Wapangaji hao wanataka mmiliki huyo asubiri kodi zao ziishe ndipo afanye ukarabati wa jengo lake.

Dar es Salaam. Wafanyabiashara 52 wa Kariakoo, jijini Da rs Salaam, wamemshtaki mmiliki wa jengo walilopanga kwa ajili ya biashara katika Baraza la Ardhi la Kata ya Kariakoo, wakipinga uamuzi wa kutaka  waondoke kabla ya mikataba yao kuisha.

 Jengo hilo la ghorofa moja ambalo juu halijakamilika, lipo block namba 18, Plot 4, mtaa wa Mchikichi, Kariakoo na  lina fremu za maduka zaidi ya  40. Awali lilikuwa likimilikiwa na Kaisi Hamis Ally, ambaye baadaye aliliuza kwa kampuni ya Phinison Investment Limited ambaye ndiye mmiliki kwa sasa.

Kampuni hiyo baada ya kununua jengo hilo, mkurugenzi wa kampuni hiyo, Salome Mgaya maarufu kama Mama Bonge, Februari 25, 2024 aliwapa taarifa ya mdomo wapangaji hao akiwataka waondoke ndani ya siku tatu kwa madai anataka kulifanyia ukarabati.

Mama bonge aliwataka wapangaji hao kuondoka katika jengo hilo Februari 28, 2024.

Hata hivyo, wapangaji hao hawakukubaliana na uamuzi huo, ndipo walipokwenda kufungua malalamiko yao katika Baraza la Ardhi la Kata dhidi ya kampuni hiyo na mmiliki wa awali wakipinga uamuzi huo.

Katika shauri hilo namba 13 la mwaka 2024, lililofunguliwa na Hubert Edwin Maleko kwa niaba ya wenzake 51, wanadai uamuzi wa mmiliki huyo wa jengo kuwataka waondoke  ndani ya muda huo ni kinyume cha mikataba yao.

Wapangaji hao wanadai mmiliki wa sasa anakiuka utaratibu, kwa kuwa wao wana mikataba halali na bado haijaisha.

Baadhi ya wapangaji wa Kariakoo, jijini Da re Salaam ambao wamemshtaki mmiliki wa jengo walilopanga vyumba vya biashara, katika  Baraza la Ardhi la Kata ya Kariakoo wakiwa katika  ofisi za baraza hilo, zilizopo Arnautoglo, Mmazi Mmoja, baada ya kufanya majadiliano na mmiliki huyo

Shauri hilo lililonguliwa Februri 27, 2024, na leo Alhamisi Machi 7, 2024 limeendelea kusikilizwa na mmiliki huyo akawapa miezi miwili badala ya siku tatu za awali.

Pia amesema baada ya ukarabati watarudi, lakini kwa kodi mpya, yaani kodi itaongezeka kutoka waliyokuwa wakilipa Sh 840,000 hadi Sh1.5milioni kwa mwezi, hivyo kodi yao iliyobaki wataongezea katika kodi mpya.

Hata hivyo, wapangaji hao wamekataa muda huo wa miezi miwili wakitaka asubiri mikataba yao iishe na kwamba hawahitaji kulipwa fidia.

Kutokana na mvutano huo, mwenyekiti wa baraza hilo, Daudi Simba ameahirisha shauri hilo hadi Machi 12, 2024 kwa ajili ya kuendelea na majadiliano na ametoa hati ya kumuita mmiliki wa zamani wa jengo hilo, Kais Ally.

Akizungumza na Mwananchi Digital baada ya kutoka kwenye majadiliano hayo, Maleko amesema mkataba huo waliongia na mmiliki wa zamani, Ally, walilipa kodi ya mwaka mmoja kuanzia Novemba 9, 2023 hadi Novemba 8, 2024.

Pia wapo wengine waliolipa kodi ya miezi sita ambayo inatarajia kuisha Julai mwaka huu.

Amesema kuwa katika fremu hizo za maduka, mpangaji mmoja analipa kodi ya Sh 840,000 kwa mwezi, huku mpangaji wa stoo analipa Sh 250,000 kwa mwezi, wakati mpangaji wa vigoro (kizimba) analipa Sh 300,000 kwa mwezi na kodi hizo wanatakiwa kulipa kwa miezi sita au mwaka mmoja.

“Mimi kodi yangu ya fremu ni Sh 840,000 kwa mwezi na nimelipa kodi ya miezi 12 ambayo ni Sh 10.8 milioni, sasa ukinipa miezi miwili ili nikupishe katika jengo lako, hiyo kodi ya miezi mingine itakuwaje?” amehoji Maleko.

Akizungumzia pendekezo la mmiliki huyo kuwapa miezi miwili, mmoja wa wapangaji, David Mwandete amesema hawajkubaliani, bali wanataka aheshimu mkataba wa wapangaji.

Kwa upande wake, Jenipher Shoo, amedai iwapo mmiliki huyo atashindwa kukubaliana na wapangaji wake kwa kuwaruhusu wamalize mkataba wao, wataliomba baraza hilo liwaandikie barua, ili waende mbele kwa hatua zaidi.