Wafanyabiashara Coco Beach waeleza magumu ya kimbunga Hidaya

Mfanyabiashara wa  Mihogo ufukuwe wa Coco Beach,Rabia Mshana, maarufu  Mama Bonge akimuhudumia mteja. Picha na Tuzo Mapunda

Muktasari:

  • Wafanyabiashara wa fukwe ya Coco Beach waeleza magumu waliyopitia siku mbili za hekaheka za kimbunga Hidaya, washusha pumzi na tabasamu na furaha yaanza kutamalaki baada ya TMA kueleza kuwa Hidaya chapunguza  makali.

Dar es Salaam. Wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao eneo la Coco  Beach wameeleza magumu ya  kimbunga Hidaya kilivyodhoofisha biashara zao baada ya wateja kupungua.

Biashara zao hazikuwa zikienda sawa kama kawaida kwa sababu ule utamaduni wa watu kwenda kwenye fukwe hizo kupunga hewa haukuwepo kwa siku mbili zilizopita.

Kwa kawaida wananchi wanaokwenda kupunga hewa ni miongoni mwa wateja wa wafanyabiashara mbalimbali zikiwamo za vyakula na vinywaji kwenye maeneo ya fukwe hizo.

Wakizungumza na Mwananchi Digital kwa nyakati tofauti  wafanyabiashara hao wamesema kipindi hicho kilikuwa cha mpito na majaribu kwao,  japo tabasamu na matumaini yameanza kurejea baada ya kimbunga  'Hidaya' kupoteza nguvu yake kikitua nchi kavu kwenye kisiwa cha Mafia mkoani Pwani kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).

 Rabia Mshana, maarufu Mama bonge anayemiliki mgahawa uitwao ‘Coco Beach Mihogo' amesema siku mbili zilizopita hali ya biashara zao ilikuwa mbaya, kwani hakukuwa na wateja kama siku nyingine.

"Hasa jana Jumamosi biashara ilikuwa ngumu, hakuna wateja palikuwa peupe kabisa, sasa kwa kuwa tumezoea kufanya biashara hatuwezi kukaa  nyumbani tulikuwa tunakuja tu," amesema na kuongeza.

"Nilijipa matumaini na kuomba kimbunga kiishe ili nasi tupate riziki, unajua biashara zetu hapa tunategemea watu wanajitokeza kwenye fukwe sasa hali ilivyokuwa na tahadhari zilizokuwa zikitolewa watu walikuwa wanaogopa kuja ," amesema.

Msimamizi wa Wavuvi Camp, Roosevelt Temu amesema mwanzo wakati hali hiyo inaanza walikuwa wanajua upepo mkali lakini hawakufikiri kama ni kimbunga.

"Hadi tulipopata habari hiki ni kimbunga Hidaya, ndipo tulipata mawazo mapya lakini upepo ule ulikuwa umeambatana na vumbi unakuja kwa nguvu na kutulia mara kwa mara," amesema Temu

Amesema hawakuwa wamejipanga kabla lakini baada ya kuona hali walianza kujipanga upya, kwanza walikubaliana  na mazingira na kila  vumbi lilipokuwa linakuja walikuwa wanafuta meza na kuziweka safi muda wote.

"Japokuwa wateja walipungua sana, ila tulijitahidi kwendana na mazingira kwa kuhakikisha eneo linakuwa safi kwa sababu vumbi lilikuwa linakuja jingi, hivyo tulilazimika kufuta viti kila mara ili mteja akikaa asichafue nguo zake, ingawa ilikuwa ngumu kuzuia kila kitu," amesema.

 Temu amesema kabla ya tishio la kimbunga Hidaya walikuwa wanapata wateja hadi wengine wanakaa katika sehemu za wazi kando na bahari hiyo  kufurahia mandhari na kupiga picha.

"Ndani ya kipindi hiki wateja waliingiwa na woga kidogo  na hata waliokuwa wanakuja walikuwa wanakaa eneo moja la huku juu  tofauti na huko chini sehemu ya wazi walikozoea kukaa kutokana na kuogopa uwepo wa kimbunga hicho," amesema

Temu amesema baada tangazo la kimbunga hicho kupungua nguvu  wamejifunza ni mabadiliko ya tabianchi na wanapaswa kuendelea kujipanga zaidi.

Naye, Ramadhan Said anayefanya shughuli zake ufukweni zinazojumuisha kusaidia wanaoogelea kwenye fukwe  hizo amesema hali ilikuwa tofauti kabisa.

"Kukiwa na hali ya kawaida siku kama hizi za Jumapili tunafanya kazi muda wote, watu na familia zao wanakuja katika fukwe hizi kufurahia lakini siku mbili hizi hakukuwa na watu kabisa naona na leo hadi muda huu pamepoa sijui baadaye," amesema.

Ramadhan amesema kipindi hicho kilikuwa cha mpito kwao ilikuwa vigumu kujipatia riziki kupitia shughuli hiyo kutokana na upepe mkali, hivyo kila mtu alikuwa anahofia usalama wake.

Mwenyekiti wa wapiga picha katika ufukwe wa Coco,  Ramadhan Omari amesema biashara yao hiyo ilikuwa ngumu kwa kuwa inategemea wingi wa watu.

“Hali ikiendelea kuwa hivi labda leo tutafanya kazi, lakini siku mbili hizi ilikuwa tofauti na kawaida watu hawakuwepo kabisa,” amesema Omari aliyefanya kazi katika eneo hilo kwa miaka 30 sasa.