Wafanyabiashara Iringa walia kutozwa kodi mara mbili

Baadhi ya Wafanyabiashara wa Mkoa wa Iringa wakiwa  katika kikao na Mkuu wa Mkoa huo, Peter Serukamba.

Muktasari:

  • Wafanyabiashara mkoani Iringa wakiwemo wamiliki wa viwanda na wa mazao ya misitu, wamemueleza RC kero zinazokwamisha jitihada zao kiuchumi.

Iringa. Wafanyabiashara mkoani hapa wametoa kero zinazowakwamisha katika kufikia malengo ya kiuchumi likiwemo suala la kutozwa kodi mara mbili, mageti mengi ya ushuru na kukatika kwa umeme viwandani.

Kwenye suala la kodi, wamesema mfanyabiashara anapovuna mti kwenye msitu wa Serikali wa Saohill, amekuwa akitozwa kodi ya halmashauri na baada ya kuachana mbao au kutengeneza nguzo, hutozwa tena kodi hiyohiyo.

Wafanyabiashara hao wametoa kero hizo katika kikao kilichofanyika baina yao na mkuu wa huo, Peter Serukamba alipokutana nao kujitambulisha  Aprili 9, 2024.

Wakizungumza katika kikao hicho, wafanyabiashara wa mazao ya misitu wamesema wamekuwa wakitozwa kodi mara mbili, jambo ambalo sio sawa.

Mwenyekiti wa chama cha wapandaji miti na utunzaji wa mazingira (Moat), Godfrey Mosha amesema suala hilo limekuwa likiwakatisha wengi tamaa.

Wakitoa mfano, wamesema viwanda 27 vimefungwa wilayani Mufindi kwa sababu ya kutozwa kodi mara mbili.

“Imebidi wengine wawe wanakimbilia kununua miti kwa wananchi, mfano ukivuna gogo, linatozwa ushuru wa halmashauri, ukishachana mbao, unatozwa tena. Mti huohuo mmoja unatozwa mara mbili,” amesema Mosha.

Mfanyabiashara mwingine, Jonas Kikwa amesema kwa upande wa Wilaya ya Kilolo, changamoto kubwa imekuwa kwenye wingi wa mageti ya ushuru.

Amesema katika wilaya hiyo, kuna mageti 10, jambo ambalo limekuwa likiwapa ugumu wa kufanya biashara.

Kuhusu suala la umeme, baadhi ya wafanyabiashara hao wameliomba Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuwa wanatoa taarifa badala ya kukata umeme ghafla, na kuharibu mitambo na kuongeza gharama.

Kwa upande wa uwanja wa ndege, wafanyabiashara hao wameomba ukamilike haraka ili safari za ndege kubwa zianze tofauti na hali ya sasa.

Kutokana na malalamiko hayo, Serukamba ametoa maagizo kwa wakuu wa wilaya kuanza kushughulikia kero za wafanyabiashara hao.

Pia, amemtaka mkuu wa wilaya ya Kilolo, Jochim Nyingo kupunguza mageti ya kukusanyia ushuru.

Amewataka Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) kuhakikisha wanarekebisha barabara ambazo zina changamoto za kupitika katika kipindi cha mvua.

Ameongeza kuwa ataendelea kufuatilia ujenzi wa barabara inayotoka mjini kwenda katika hifadhi ya Ruaha na kuhakikisha ujenzi wake unakamilika.

Sambamba na hayo Serukamba ameahidi kuendelea kufuatilia na kupambana na baadhi ya changamoto kwa kuhakikisha anazitatua.