Wafanyabiashara Kibaha wataka kuboreshewa soko

Wafanyabaishara wa soko la Kongowe wakiendelea na shughuli zao. Picha na Sanjito Msafiri

Muktasari:

  • Wamesema soko lililopo linasababisha kero kubwa kwa kuwa hakuna paa la pamoja la kuzuia mvua, badala yake kila mmoja amejenga kibanda chake.

Kibaha. Wafanyabiashara katika Mtaa wa Kongowe uliopo Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani, wameomba kuboreshewa mazingira ya soko ili wafanye shughuli zao sehemu salama.

Katibu wa soko hilo, Dotto Evarist amesema leo Januari 18, 2024 kuwa kutokana na ubovu wa miundombinu, wamekuwa wakiendesha shughuli zao huku wakipitia changamoto mbalimbali ikiwemo kuloa wakati wa mvua kwa kuwa hakuna paa la pamoja

“Soko halina paa la pamoja ni vibandavibanda ambavyo vimejengwa kienyeji, kila mtu anavyoweza, sasa hali hiyo inatuwia ugumu sisi wajasiliamali. Tunaomba mamlaka husika zichukue hatua ya kutujengea soko,” amesema Evarist alipozungumza na Mwananchi Digital.

Amesema kwa sasa wanafanya biashara kwenye eneo ambalo sio rasmi na wakati wa mvua bidhaa zao zinanyeshewa, hivyo kuwa hatarini kuharibika na kusababisha hasara.

“Tumeomba Serikali itusaidie kuboresha mazingira yetu ikiwa ni pamoja na kutusogezea huduma ya maji, umeme na choo na kutujengea vizimba vya biashara, ili tufanye shughuli zetu katika sehemu nzuri wakati wakitutafutia eneo la kudumu,” amesema.

Katibu huyo ameongeza kuwa ni vema mamlaka itakapoamua kutenga eneo litakalojengwa soko lisiwe mbali na makazi ya watu, ili wateja wawafikie kwa urahisi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kongowe, Maimuna Jamhuri amekiri kutokuwapo kwa soko kwenye mtaa wake na kwamba sasa wafanyabiashara hao wanafanya shughuli zao kwenye eneo lisilo rasmi.

Amesema katika mambo wanayoendelea kuyafanyia kazi kwa sasa ukiachilia soko, ni pamoja na miundombinu ya barabara ambayo mengi yameharibika, hivyo kusababisha kutopitika.

Akizungumzia kero ya soko, diwani wa kata ya Kongowe, Hamis Shomari amesema halmashauri ya Kibaha ina mpango wa kulikarabati kwa kujenga paa na vizimba, ili wananchi wafanye biashara kwenye mazingira bora.