Wafanyakazi Dodoma walia na Tume ya Utumishi wa Umma

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Jumanne Sagini akizungumza katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Leo Mei 1,2023 jijini Dodoma

Muktasari:

  • Tume ya utumishi wa umma yatajwa kusababisha wafanyakazi kufukuzwa kazi. Hii ni kutokana na baadhi ya watumishi kushinda rufaa zao lakini Tume imekuwa ikitoa tena mwanya kurudiwa kwa mashauri hayo na waajiri.

Dodoma. Katika kuadhimisha siku ya wafanyakazi, Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) limeeleza kushangazwa na suala la Tume ya Utumishi wa Umma kuwapa nafasi ya kukata rufaa waajiri wanaposhindwa kesi dhidi ya wafanyakazi wao.

Hali hiyo imeelezwa kusababisha wafanyakazi kufukuzwa kazi baada ya kutoa mwanya kwa waajiri kurudia usikilizwaji wa mashauri hayo.

Hayo yameelezwa leo Mei 1, 2023 na Dk Leonia Msafiri, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Mkoa wa Dodoma wakati akisoma risala kwa Naibu Waziri wa mambo ya ndani Jumanne Sagini katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi, Jijini Dodoma.

“Kuna baadhi ya watumishi rufaa zao zinashinda na Tume inaamua kutengua uamuzi wa waajiri lakini cha kushangaza katika barua hiyohiyo Tume inawaelekeza waajiri kurudia au kuanzisha upya mchakato wa shauri la kinidhamu, hii inadhihirisha kwamba Tume inaungana na mwajiri kuhakikisha wafanyakazi wanafukuzwa kazi,”amesema.

Hata hivyo akizungumza baada ya kusikiliza risala hiyo Naibu Waziri wa mambo ya ndani Jumanne Sagini alifafanua kuwa Tume hiyo haina lengo la kusababisha wao kufukuzwa kazi bali kujiridhisha katika upatikanaji wa haki kwa pande zote mbili.

“Katika risala yenu mmeikosoa Tume ya Utumishi wa umma kama chombo cha rufaaa cha juu kwamba vile wana dhamira ya kuona mnafukuzwa kazi kwasababu ya kutaka michakato ya nidhamu ianze upya, si kwamba wanataka mfukuzwe bali ni kutaka sheria izingatiwe na haki itolewe kwa mfanyakazi.

Sagini ameongeza kuwa, kama mfanyakazi atakutwa hatia hatafukuzwa kazi, hiyo nayo ni haki yake


Aidha katika risala yake Dk Leonia ametaja changamoto za wafanyakazi kutolipiwa stahiki zao kwenye mifuko ya wafanyakazi, kupewa mishahara isiyoendana na hali ya maisha, kuondolewa kwa wafanyakazi kwenye vyama vyao kinyume na utaratibu na kuchaguliwa vyama vya kujiunga na waajiri wao.


Mwisho.