Wafanyakazi wa majumbani wacharuka

Muktasari:

  • Wafanyakazi wa majumbani wameomba mkataba namba 189 uridhiwe na Serikali, huku wakiwaomba waajiri wao kuwaheshimu, kwani wao ni zaidi ya walezi katika familia.

Dodoma. Wafanyakazi wa majumbani wameomba mkataba namba 189 uridhiwe na Serikali, huku wakiwaomba waajiri wao kuwaheshimu, kwani wao ni zaidi ya walezi katika familia.

Kilio hicho wamekitoa juzi, walipokuwa wakizungumza kwenye mkutano wa wafanyakazi wa majumbani ulioandaliwa na Chama cha Wafanyakazi wa mahotelini, mashambani na majumbani (Chodawu).

Akizungumza katika mkutano huo, Mariamu Mwaramu alisema changamoto kubwa ambazo wamekuwa wakikutana nazo ni pamoja na kutoheshimiwa, kutopewa muda wa mapumziko, udhalilishwaji wa kingono, kutopewa likizo ya uzazi, kutoaminiwa, kutopewa mshahara kwa wakati na kukashifiwa.

“Hatuna Jumapili wala Jumamosi, muda wote sisi ni kufanya kazi, ukisema nikaangalie ndugu ni shida, mshahara wenyewe hupati kwa wakati, ukisema uombe shida inaanzia hapo hapo,” alisema.

Hata hivyo ameiomba Serikali kuridhia mkataba namba 189 kwani una vitu vingi vitakavyowafanya wapate baadhi ya haki zao. Miongoni mwa haki ambazo zinatajwa kwenye mkataba huo ni pamoja na: kuheshimiwa, kupewa muda wa kupumzika na likizo, kulipwa kwa wakati pamoja na haki ya kusikilizwa kama ilivyo kwa wafanyakazi wengine.

Hata hivyo, baadhi ya vipengele kwenye mkataba huo vinaonekana kutoendana na mazingira halisi ya Tanzania ikiwemo mwajiri kumtengea chumba kulala na mwenza wake pamoja na kutumika kama dereva wa familia.

Kwa upande wa Beatrice John ambaye anafanya kazi za ndani mkoani Morogoro alisema wamekuwa hawathaminiki katika jamii hadi kufikia kupewa majina ya udhalilishaji kama beki tatu.

“Tumesahaulika, tunaomba tusikilizwe hata kidogo, mkataba uridhiwe ili tutambulike.Sisi ni walimu, sisi ni madaktari japokuwa hatuna vyeti, watoto wakianza kuumwa sisi ndio huwa tunaanza kuwahudumia, tunaomba tuheshimike,” alisema.

Naye Katibu Mkuu wa Chodawu Tanzania Bara, Said Wamba alisema wanaiomba Serikali iweke sheria madhubuti kwa wafanyakazi wa majumbani kwani ni watu muhimu katika jamii.

Wamba alitoa rai kwa wafanyakazi wa majumbani kujiunga na chama hicho ili iwe rahisi kutetea maslahi yao pamoja na kupaza sauti kwa chochote kitakachowatokea wakiwa kazini.


Sheria inasemaje?

Kamishna wa kazi Msaidizi, Rehema Moyo alisema sheria iliyopo ni ya ajira na mahusiano kazini sura 366. Alisema haki zilizoainishwa chini ya sheria hiyo ni mikataba ya kazi, kupewa likizo, saa za kazi, haki ya kulipwa mishahara na kujiunga na vyama vya wafanyakazi.