Wahadhiri UDSM wachambua mambo 53 ripoti Jaji Chande, watahadharisha yasijirudie
Muktasari:
- Katika taarifa yao wanazuoni hao wamechambua masuala yaliyopo katika wasilisho la Jaji Chade, alilotoa Aprili 23, mwaka huu mbele Rais Samia Suluhu Hassan, wakisema walitamani sana kupata taarifa kamili ili kufanya uchambuzi wa kina. Kwa bahati mbaya ripoti hiyo bado haijatolewa na hivyo kukosa fursa ya kuisoma.
Dar es Salaam. Wakati mjadala wa Tume ya uchunguzi wa matukio ya Oktoba 29 ukiendelea, Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udasa), imetaja mambo 53 iliyoyabaini katika wasilisho la Tume hiyo.
Kutokana na wasilisho la Tume hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Mohammed Chande Othman, Fikira za Udasa ni kwamba msingi wa amani na utulivu katika nchi yetu ya Tanzania ni haki, usawa, uwajibikaji, kuheshimu haki za binadamu na utawala bora, ambavyo kwa ujumla wake vitajenga imani ya wananchi kwa Serikali na viongozi wao, wamesema.
“Kila raia na mkazi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ana wajibu na mchango katika kuhakikisha tunalinda amani na kujenga mshikamao wa kitaifa,” ilieleza taarifa hiyo ya Aprili 28, 2026 iliyosainiwa na Mwenyekiti wa Udasa, Elgidius Ichumbaki.
Katika taarifa yao wanazuoni hao walichambua masuala yaliyopo katika wasilisho la Chade, wakisema ilitamani sana kupata taarifa kamili ili kufanya uchambuzi wa kina lakini kwa bahati mbaya ripoti hiyo bado haijatolewa na hivyo kukosa fursa ya kuisoma.
“Hata hivyo, kama sehemu ya kutekeleza wajibu wetu wa kisomi kwa jamii, imetubidi kumulika wasilisho la Jaji Chande na kutoa tafakuri yetu. Hivyo basi, hii ni tafakuri ya Udasa kuhusu wasilisho la Jaji Chande alilolifanya mbele ya Rais na viongozi waandamizi wa Serikali,” ilieleza taarifa hiyo.
Udasa imesema kutokana na wasilisho la Chande kuna masuala 53 ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi ili kuepuesha masuala yaliyojitokeza katika uchanguzi mkuu wa mwaka jana.
Hata hivyo masuala hayo yaliyomengi yalikuwa yametolewa na Tume kwa ujumla na kilichofanywa na udasa ni kuyanyumbulisha na kuyatafsiri.
Hoja za Udasa
Miongoni mwa masuala hayo ni kukosekana kwa Katiba Mpya yenye kukidhi matakwa ya wananchi na kukosekana tume huru ya kusimamia uchaguzi.
Nyingine zilizotajwa na wote ni watu kutekwa na kupotea, ukosefu wa ajira hasa kwa vijana, changamoto za kidemokrasia, kudorora kwa uchumi wa wananchi hasa vijana na kupungua kwa uzalendo.
Mbali na hizo, Udasa kupitia uchambuzi wake, imetaja masuala mengine kuwa ni Jeshi la Polisi kutokutenda haki na kushindwa kutimiza majukumu yake ya kulinda usalama wa raia na mali zao.
“Serikali kutokuwasikiliza wananchi na kutatua kero au changamoto zao, viongozi waandamizi wa Serikali kushindwa kutimiza majukumu yao kikamilifu na kukosekana vyombo vya habari huru na vyenye kutoa tahariri za kina, zinazofuata misingi ya weledi ili kuuhabarisha umma na Serikali juu ya mambo ya msingi yanayoendelea kuleta sintofahamu,” imesema.
Vilevile ni hasira za wananchi kwa viongozi wa Serikali wasiotimiza wajibu wao kikamilifu, Jeshi la Uhamiaji kushindwa kutimiza wajibu wake kikamilifu na baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi kutumia nguvu kupita kiasi.
Pia, Udasa imetaja baadhi ya watu kukichukia chama tawala, watu kutoridhishwa na kukosa imani na utendaji wa Mahakama na watumishi wa Serikali kuwa na kiburi na kushindwa kuwahudumia wananchi kikamilifu.
Suala lingine ni Msajili wa Vyama vya Siasa na Tume Huru ya Uchaguzi kushindwa kushughulikia kero na malalamiko ya vyama vya siasa na ya wananchi kwa ujumla na wasomi kutotimiza wajibu wao, kukosekana mifumo ya ajira za ushindani, uhusiano mbaya wa polisi na wananchi, kutowajibika kwa viongozi wa Serikali na kukosekana mifumo duni ya kusimamia utekelezaji wa sheria.
Udasa, imetaja kuwa kukosekana kwa sekta binafsi imara na yenye kuwezesha upatikanaji wa fursa miongoni mwa vijana kama ajira na mikopo lakini pia kupungua kwa mshikamano na kuaminiana miongoni mwa wananchi, watumishi kutoridhishwa na mazingira ya kazi, kukosekana kwa uwajibikaji au uwajibishwaji kwa muda muafaka.
Pia, imesema ni Serikali kuwa na matumizi ya hovyo, yasiyozingatia vipaumbele, wananchi kupoteza imani na mifumo ya kijamii na ya kisiasa, watu wengi hasa vijana kukata tamaa ya maisha na kusababisha miongoni mwao kuwa na matatizo ya afya ya akili.
“Serikali kushindwa kuchukua hatua stahiki na kwa haraka ili kutatua kero za wananchi ikiwemo kutekeleza mapendekezo yanayotolewa na vyombo vyake yenyewe kama vile tume na vikosi kazi mahsusi,” imesema.
Udasa, imesema uongo unaotolewa na viongozi wa kisiasa na Serikali, Serikali kushindwa kusikiliza ushauri wa wataalamu, busara za wazee na viongozi wa kidini, kukosekana au kupungua kwa rasilimali fedha na rasilimali watu katika taasisi mahsusi za kutoa huduma za kijamii kama hospitali na zimamoto.
“Chama cha Mapinduzi kushindwa kuwa na intelijensia na akili kubwa ya kukisaidia kuona mbali na kufanya siasa zenye kufuata misingi ya haki na utu na viongozi wa Serikali kuwa wezi na wabadhirifu wa mali za umma na kuishi maisha ya anasa,” imesema.
Imetaja masuala mengine kuwa ni vyombo na taasisi mbalimbali za Serikali kushindwa kutimiza wajibu wake kwa kufuata sheria, kukithiri kwa vitendo vya rushwa na ufisadi na kukosekana kwa ukweli na uwazi katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kitaifa.
Pia, Bunge kushindwa kutimiza wajibu wake wa kuisimamia na kuiwajibisha Serikali na vyombo vyake, Serikali na vyombo vyake kushindwa kufanya upelelezi wa haraka, huru, stahiki na kamilifu na kuwachukulia hatua maofisa wa polisi wanaokiuka viapo vyao.
Jingine ni mgawanyiko usiokuwa wa wazi na kutokuelewana au kutofautiana baina ya taasisi za Serikali na viongozi wakuu wa Serikali na vyombo vyake.
“Baadhi ya vyombo vya Serikali kuchelewa kuchukua hatua stahiki hata pale ambapo vinapata taarifa za kuaminika kuhusu tishio fulani na kuongezeka kwa nyufa katika umoja na mshikamano wa kitaifa na majeraha ya muda mrefu ya baadhi ya wananchi,” imesema.
Pia, imetaja kupungua kwa utulivu wa kisiasa na kijamii na kuwa mbinu za kiutendaji na kutatua kero za wananchi haziendani na kasi ya vijana, Serikali na vyombo vyake vya dola kushindwa kutimiza majukumu yake kwa uwazi na kufuata demokrasia ya vyama vingi vya siasa.
“Serikali na taasisi zake kushindwa kusimamia maadili ya viongozi wa umma na wa kisiasa jambo ambalo limepelekea kukiuka miiko na taratibu za kiutumishi,” imesema.
Kadhalika udasa ilitaja sauala la wananchi kuhisi kupoteza nguvu yao ya kuchagua viongozi, kuwepo utitiri wa kodi na vyombo vya usimamizi vinavyoingiliana kimajukumu, kuongezeka kwa kiwango cha umaskini na mmomonyoko wa maadili.
Udasa, imesema msingi wa amani na utulivu Tanzania ni haki, usawa, uwajibikaji, kuheshimu haki za binadamu na utawala bora ambavyo kwa ujumla wake vitajenga imani ya wananchi kwa Serikali na viongozi wao.
“Mambo ambayo tumeyataja ambayo yanatokana na wasilisho la Jaji Chande yanatakiwa kupatiwa ufumbuzi siyo na Serikali na vyombo vyake pekee, bali kila raia na mkazi Tanzania ana wajibu na mchango katika kuhakikisha tunalinda amani na kujenga mshikamao wa kitaifa,” imesema.