Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wahariri wapinga Serikali kujiingiza Bodi ya Ithibati

Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena

Muktasari:

Wanataaluma hao wamesema iwapo bodi hiyo ya kitaaluma haitaingizwa mkono wa Serikali katika uundwaji wake, Serikali itapata sehemu ya kwenda kupeleka malalamiko yake pale itakapokwazwa na mwanahabari.

Dar es Salaam. Wahariri wa vyombo vya habari nchini, wameeleza kwamba, uundwaji wa Bodi ya Ithibati ya Habari huru utaweka mazingira ya usawa kati ya Serikali na vyombo vya habari nchini.

Wameeleza kuwa, iwapo bodi hiyo ya kitaaluma haitaingizwa mkono wa Serikali katika uundwaji wake, Serikali itapata sehemu ya kwenda kupeleka malalamiko yake pale itakapokwazwa na habari au mwanahabari.

Kauli hiyo imekuja kufuatia maoni ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Eliezer Feleshi aliyoyatoa Mei 13, 2022 alipokutana na wadau wa habari ofisini kwake bungeni, jijini Dodoma.

Mei 31, 2021, aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa (kabla tasnia ya Habari kuhamishiwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Tasnia ya Habari) alisema Serikali inaendelea na taratibu za kuanzisha bodi ya ithibati itayokuwa na jukumu la kutoa ithibati na vitambulisho kwa wanahabari wenye sifa.

Bashungwa, ambaye sasa ni Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Tamisemi), alitoa kauli hiyo wakati akiwasilisha makadiro ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Wakizungumza leo Julai 12 jijini Dar es Salaam katika mkutano wa wadau wa habari, wahariri hao wamesema kuundwa kwa chombo hicho, kutakuwa mwarobaini wa malalamiko ya muda mrefu kutoka kwenye vyumba vya habari mbalimbali nchini.

Neville Meena, Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) amesema iwapo Serikali itaamua kuunda Bodi ya Ithibati ya Habari, basi bodi hiyo itakosa uhuru wa kufanya uamuzi pale malalamiko yatakapoihusu yenyewe (Serikali).

Amesema, ili kukwepa hilo na kutenda haki kwa vyombo vyote vya habari nchini, hakuna budi kwa Bodi ya Ithibati ya Habari kuundwa na kusimamiwa na wanataaluma wenyewe ambao ndio wanahabari.

“Bodi ya Ithibati ya Habari ikisimamiwa na Serikali, itakosa uhuru wa kuamua, hivyo inapaswa kuundwa na wanataaluma na kazi yake ni ya kitaaluma. Serikali ikiwa na malalamiko nayo inakwenda kulalamika kwenye bodi na wala haipaswi kutoa maelekezo,” ameeleza Meena.

Kwa upande wake, Mhariri wa Gazeti la Raia Mwema, Joseph Kulangwa alionyesha wasiwasi iwapo serikali itasimamia uundwaji wa bodi hiyo akisema, “serikali itataka wanaowaandika vizuri tu, ndio wahalalishwe kufanya kazi hiyo.”

Alisema, tasnia mbalimbali nchini zimeunda na kusimamia bodi zao wenyewe bila maelekezo ama kuingiliwa na Serikali, amehoji sababu za Serikali kupendekeza kuunda bodi hiyo badala ya kuwaacha wanataaluma wa habari kuunda na kusimamia bodi hiyo.

Naye Jimmy Charles, Mhariri wa Jarida la Tz & Beyond pia Panaroma alisema, iwapo Serikali itaunda bodi hiyo, itajihakikishia uhuru wa habari kutuama mikononi mwake.