Wahitimu UDSM wahimizwa kujitolea, kujiajiri

Muktasari:

 Jumla ya wahitimu 3,213 asilimia 52 wakiwa ni wanawake na asilimia 48 wanaume wametunukiwa shahada za awali, stashahada na astashahada katika mahafali ya 52 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.



Dar es Salaam. Jumla ya wahitimu 3,213 asilimia 52 wakiwa ni wanawake na asilimia 48 wanaume wametunukiwa shahada za awali, stashahada na astashahada katika mahafali ya 52 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Kati ya wahitimu hao wapo 15 ambao ni kundi la kwanza la wanufaika wa ufadhili wa masomo unaotolewa na chuo hicho kwa wanafunzi waliofanya vizuri zaidi kwenye masomo ya sayansi katika mitihani yao ya kidato cha sita na kuchaguliwa kujiunga na UDSM katika shahada ya awali.


Akizungumza wakati wa mahafali hayo Makamu Mkuu wa chuo hicho Profesa William Anangisye amewataka wahitimu hao kutumia elimu waliyopata kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii na kuleta mabadiliko chanya.


Pia Profesa Anangisye amewataka wahitimu hao kuachana na mawazo ya kuajiriwa na badala yake kutafuta namna bora za kutumia ujuzi waliopata.


“Elimu mliyoipata ni mali ya umma hivyo ni lazima ilete faida kwa umma wa Watanzania. Elimu haiwezi kuwa chachu ya mabadiliko kama haitatumika changamoto zilizopo kwenye jamii. Msisubiri kuajiriwa angalieni sehemu ambayo ujuzi wenu unaweza kutumika hata kama kwa kufanya kazi kwa kujitolea.


“Ni muhimu mkawa wepesi kujifunza mambo mapya nanyi mkabadilika kwa haraka ili msiachwe na wakati, mkawe chachu ya maendeleo na mfano wa kuigwa. Muwe watu wa kutafuta fursa badala ya kusubiri fursa ziwafuate jambo ambalo si rahisi katika ulimwengu wa leo,”amesema Profesa Anangisye.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Balozi Mwanaidi Maajar amewataka wahitimu hao kuwa mabalozi wazuri wa chuo hicho na kujiepusha na vitendo ambavyo vinaweza kuleta taswira mbaya kwao na chuo.