Wahitimu watakiwa kukumbatia Tehama

Rais wa Baraza la Chuo Cha Mtakatifu Joseph, Dk Thomson Ananth (katikati), akikadhidhi zawadi kwa mmoja ya wahitimu katika Mahafali ya 16 ya chuo hicho yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Wahitimu kutoka Chuo cha Mtakatifu  Joseph wanajivunia mafunzo ya Tehama, wasema wana uwezo mkubwa wa kujiajiri na kuajiri.

Dar es Salaam. Rais wa baraza la Chuo cha Mtakatifu Joseph, Dk Thomson Ananth amewataka wahitimu  kutoka chuoni hapo kuikumbatia Tehama.

Dk Thomson ametoa rai hiyo leo Desemba 13, 2023 kwenye mahafli ya 16 yaliyofanyika chuoni hapo.

Katika mahafali hayo wahitimu 416 wa ngazi za Shahada na Stashahada walitunukiwa vyeti.

Amesema  nidhamu na elimu ikihusisha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) waliyoipata wakaitumie kujisaidia wao na jamii kwa ujumla.

"Teknolojia inabadilika kila siku, mnapaswa kuwa macho. Mjifunze zaidi ili mkawe msaada kwenye  ustawi wa Taifa katika nyanja mbalimbali," amesema.

Amesema baraza linatilia mkazo kukuza uwezo wa wahitimu wa kukabiliana na changamoto za dharura zinazotokea duniani kwa kutoa elimu bora inayoleta maendeleo nchini.

"Ili kutimiza azma hiyo, baraza kupitia menejimenti ya chuo limeweka sera ya teknolojia na  biashara, ambayo ilianzisha kituo cha kuongeza kasi ya ubunifu na teknolojia (ITAF), kupitia hilo kimeendelea kuibua vipaji vya wanafunzi na mawazo ya kibunifu," amesema.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Eliab Opiyo amesema wanawaandaa wanafunzi kuwa tayari kwenye soko la ajira ili wamudu  kujitegemea.

"Tunasisitiza zaidi katika vitendo. Wanakwenda viwandani, hospitalini, shuleni kwa mafunzo ya vitendo ili watakapotoka hapa waweze kuingia kwenye soko la ajira," amesema.

Mmoja wa wahitimu, ambaye ni mwanafunzi bora wa Shahada ya Uhandisi wa Majengo na Barabara, Dickson Pello amesema Tehama kwa sasa inatumika kila mahali.

Amesema amejipanga kwenda kuitumia elimu ya teknolojia aliyopata kuisaidia jamii katika ukuaji kwenye sekta ya ujenzi.

"Soko la ajira lina ushindani na unategemea kila mmoja wetu jinsi anavyojitoa. Mfumo wa sasa unahusisha matumizi ya kompyuta na akili bandia (AI), haijalishi upo sekta gani,  hivyo nawasihi wanafunzi wenzagu wawekeze nguvu kwenye Tehama," amesema.

Naye Julieth Bomani, mhitimu wa Shahada ya Uhandisi wa Majengo na Barabara, amesema anaweza kujiajiri na kuajiri wengine kutokana na elimu aliyoipata ikihusisha matumizi ya Tehama.

Akizungumzia changamoto ya ajira, muhitimu wa Shahada ya Udaktari wa Binadamu, Awadh Athumani amesema ili kukabiliana nayo ni kujifunza ujuzi zaidi.

"Lazima ujiongeze, ndiyo maana tunajitahidi kujifunza ujuzi mbalimbali. Ukiangalia kwa sasa taarifa nyingi za hospitali zinatunzwa kwenye kompyuta na mifumo ya Tehama ndiyo inayotumika, hivyo lazima ufahamu mambo yote haya ili uwe na  thamani kwenye soko la ajira," amesema.