Wajasiriamali kutoka nchi sita kukutana Mwanza

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Wajasiriamali kutoka nchi sita za Afrika Mashariki wanatarajia kufanya maonesho ya bidhaa zao Desemba 2 hadi 12 mwaka huu katika viwanja vya Rock city mall jijini Mwanza.

Mwanza. Zaidi ya wajasiriamali 1,050 kutoka nchi sita za Afrika Mashariki watakutana jijini Mwanza Desemba 2 hadi 12 katika maonesho ya 21 ya nguvu kazi /jua kali lengo likiwa ni kuwawezesha kurasimisha shuguli zao kwa kupatiwa fursa za kutangaza bidhaa zao.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel amesema maonesho hayo ya wajasiriamali pia yatawawezesha kubadilishana taarifa, kukuza ujuzi, kukuza masoko ya bidhaa na kukuza teknolojia ya utengenezaji wa bidhaa na hatimaye kuongeza furasa za ajira kwa vijana.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa ofisi yake, Gabriel amesema maonesho hayo yanayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na ofisi ya Mkoa wa Mwanza, yataenda sambamba na makongamano ya kuwajengea uwezo wajasiriamali na wabunifu kuhusu masoko, ubora wa bidhaa, urasimishaji biashara na kuongeza thamani ya bidhaa.

Amewataka wajasiriamali nchini na mikoa ya Kanda ya ziwa kujitokeza kuonesha bidhaa zao kwakuwa ni fursa kwao kujifunza mbinu za kutengeneza bidhaa na kutafuta masoko kutoka kwa wajasiriamali wa nchi zitakazoshiriki maonesho hayo.

“Maonesho hayo yanaenda sambamba na maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru pamoja na maonesho ya kazi za wahandisi na ubunifu wa mkoa wa Mwanza hivyo vijana wetu zaidi ya 50 wataitumia fursa hii kuonesha kazi zao za ubunifu katika sekta ya teknolojia ya habari, viwanda, kilimo, biashara na huduma za kijamii ikiwemo Elimu na Afya,”amesema Gabriel

Amewaomba wananchi wa Mkoa wa Mwanza na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki kama wabunifu au kutembelea maonesho ili wajionee na kujifunza huku akidai ofisi yake imezielekeza Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuhakikisha vijana wabunifu na wajasiriamali watakaoshiriki maonesho hayo wanapeleka bidhaa za asili za Mikoa, Wilaya au Mitaa wanayotoka.

“Fomu za maombi pamoja na maelekezo kwa wajasiriamali na wabunifu wanaokusuidia kushiriki maonesho hayo zinapatikana kupitia ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mwanza kupitia kwa ofisa biashara wa sektarieti ya Mkoa wa Mwanza, ofisi za Maofisa biashara kwenye halmashauri zote nchini, Ofisi zote za Mameneja wa Shirika la Viwanda Vidogo nchini (Sido) na mwisho wa kurudisha fomu ni Novemba 28 mwaka huu ili kutoa fursa kamati kuchagua wajasiriamali wanaokidhi vigezo”amesema

Mjasiriamali wa viatu vya ngozi Mtaa wa Lumumba jijini Mwanza, Rebeka Nestory amesema uwepo wa maonesho hayo utatanua wigo wa biashara kati yao na wenzao kutoka sehemu mbalimbali nchini na nje ya nchi.