Wakazi Dar watandika kanga barabarani wakimuaga Magufuli

Wakazi Dar watandika kanga barabarani wakimuaga Magufuli

Muktasari:

Wapo waliotandika kanga na vitenge barabarani wakati gari lililobeba jeneza la aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli likipita kwenda katika Uwanja wa Uhuru inakofanyika ibada ya kuaga mwili wa kiongozi huyo.

Dar es Salaam. Wapo waliotandika kanga na vitenge barabarani wakati gari lililobeba jeneza la aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli likipita kwenda katika Uwanja wa Uhuru inakofanyika ibada ya kuaga mwili wa kiongozi huyo.

Wengine walikuwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali kuhusu kiongozi huyo aliyefariki dunia Machi 17, 2021.

Baada ya ibada ya kuaga iliyofanyika katika Kanisa la St Peters, msafara wa magari kuelekea Uwanja wa Uhuru ulipita barabara mbalimbali ambapo wananchi walikuwa wamejipanga pembezoni na katika kuonyesha mapenzi yao kwa Magufuli walidiriki kuingia katikati ya barabara na kutandika vitenge na kanga hizo huku wakilia.

Wakati vilio vikitawala kila barabara ambayo msafara wenye mwili wake ulipita  kuanzia eneo la Morocco, Kinondoni, Magomeni, Ilala na Chang’ombe, baadhi ya wananchi walikuwa na mabango hayo.

Baadhi ya mabango hayo yalisomeka, Kwaheri Jemedari wetu, R.I.P chuma mtetezi wa wanyonge, R.I.P JPM chuma cha Afrika.

Katika baadhi ya maeneo wananchi waliishiwa nguvu na kuketi chini na baadhi kuanguka, maeneo yaliyokuwa na watu wengi zaidi ni Ilala lilipo soko la wamachinga hadi Chang’ombe na wengine waliingilia msafara wake na pikipiki.