Wakazi Tangasisi walia adha ya mafuriko, waiomba Serikali iwasaidie
Wakazi wa Mtaa wa Tangasisi, jijini Tanga, wakilazimika kupita kwenye maji yaliyofurika kuingia katika makazi yao yaliyogubikwa na mafuriko.
Muktasari:
- Wakazi wa Mtaa wa Tangasisi, jijini Tanga, wameiomba serikali kuingilia kati tatizo sugu la maji ya mvua kutuama katika makazi yao, hali inayosababisha hasara, kuhatarisha afya na kuathiri maisha ya kila siku, huku wakisisitiza umuhimu wa kujengwa kwa mifereji ya kudumu.
Tanga. Kila mvua inaponyesha, wakazi wa Mtaa wa Tangasisi jijini Tanga hulazimika kuanza upya mapambano ya kuokoa maisha yao na mali zao hali ambayo sasa wameichoka na kuiomba Serikali iingilie kati kwa suluhisho la kudumu.
Wananchi hao wanasema maji ya mvua hutua na kutuama kwa muda mrefu kwenye makazi yao, yakisababisha hasara kubwa, kuhatarisha afya na kuvuruga maisha ya kila siku, huku wakisisitiza kuwa ujenzi wa mifereji ya kudumu ndiyo suluhisho pekee.
Mwandishi wa Mwananchi alipotembelea eneo hilo Mei 5, 2026, alishuhudia hali halisi ilivyo mbaya, huku baadhi ya wakazi wakidai hulazimika kukaa juu ya dari za nyumba zao wakati maji yanapofurika ndani.
Maji yaliyotuama katika makazi ya wakazi wa Mtaa wa Tangasisi, jijini Tanga, yakitoa harufu kali kufuatia kujaa takataka zilizosombwa na mvua kutoka maeneo mbalimbali ya kata hiyo.
Mkazi wa eneo hilo, Munuwani Ally, amesema ameishi Tangasisi kwa zaidi ya miaka 10, lakini kila msimu wa mvua changamoto hiyo hurudia bila ufumbuzi wa kudumu.
“Wakati wa mvua tunakosa kabisa amani. Maji yanaingia ndani hadi kulazimika kupanda juu. Tumeomba msaada mara nyingi lakini bado hakuna hatua madhubuti,” amesema.
Kwa upande wake, Saumu Salimu Ally amesema hali hiyo huathiri hata miundombinu ya msingi kama vyoo, hali inayosababisha uchafu kusambaa na kuongeza hatari ya magonjwa ya mlipuko.
“Hapa tunaishi kwenye mateso. Vyoo vinaziba, maji yanachanganyika na uchafu. Serikali ikiweka mifereji mikubwa tu, tatizo linaweza kuisha,” amesema Saumu.
Naye Fatuma Said amesema eneo hilo limekuwa na hofu ya kudumu kila msimu wa mvua unapokaribia, akibainisha kuwa maji hayo hubeba taka mbalimbali kutoka maeneo ya jirani.
“Kila mahali ni maji yaliyotuama yenye uchafu mwingi. Tunahofia sana magonjwa kama kipindupindu. Hii ni hatari kwa maisha yetu,” amesema Fatuma.
Mkazi wa Mtaa wa Tangasisi, jijini Tanga, wakilazimika kupita kwenye maji yaliyofurika kuingia katika makazi yao yaliyogubikwa na mafuriko.
Hasara za kiuchumi pia zimekuwa kubwa, huku mifugo kama kuku ikifa kutokana na kukosa sehemu salama.
Akithibitisha hilo Elizabeth Mohamed amesema tayari amepoteza kuku 15 kati ya 50 aliokuwa anawafuga.
“Nyumba imejaa maji, hata banda la kuku limefurika. Hii hali haiwezi kuendelea. Serikali ikiweka makaravati na mifereji tatizo linaisha,” amesema Elizabeth.
Kwa mujibu wa wakazi hao, chanzo cha tatizo hilo kinahusishwa na jiografia ya eneo hilo ambalo ni la bonde, pamoja na shughuli za awali za uchimbaji mchanga zilizobadilisha mfumo wa mtiririko wa maji.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Tangasisi, Adam Idrisa, amesema tatizo hilo ni la muda mrefu na limekuwa likijadiliwa katika vikao mbalimbali bila mafanikio.
“Eneo hili lilichimbwa mchanga kwa muda mrefu, sasa limekuwa kama hifadhi ya maji. Mvua ikinyesha, yanajaa na kusababisha mafuriko makubwa,” amesema.
Ameongeza kuwa zaidi ya nyumba 15 zimeathirika vibaya, huku tukio la awali likiwa limehusisha vifo vya watoto watatu waliodaiwa kuzama kwenye maji hayo.
“Hatuwezi kusubiri hadi madhara yaongezeke. Tayari tumepoteza watoto watatu. Tunahitaji hatua za haraka,” amesema.
Athari hizo zimegusa pia sekta ya elimu. Jabiri Malema, mkazi wa eneo hilo, amesema watoto hukosa shule kutokana na kushindwa kupita kwenye maji.
“Huwezi kumpeleka mtoto shule asubuhi wakati kila mahali kumejaa maji na uchafu. Hii inaharibu mustakabali wa elimu yao,” amesema Malema.
Akizungumzia hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dadi Kolimba, amekiri kuwepo kwa tatizo hilo na kusema Serikali inafahamu changamoto hiyo.
Amesema jitihada zinaendelea kutafuta suluhisho la kudumu, likiwemo uwezekano wa kuboresha miundombinu ya mifereji ili kuondoa maji hayo kwenye makazi ya wananchi.