Wakili afungwa jela miaka saba kwa kumuua mpenzi wake
Muktasari:
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemhukumu wakili wa kujitegemea Steven Mduma (38) kifungo cha miaka saba jela, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mpenzi wake, aitwaye Jackline Mwanjimbe.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemhukumu wakili wa kujitegemea Steven Mduma (38) kifungo cha miaka saba jela, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mpenzi wake, aitwaye Jackline Mwanjimbe.
Mduma anadaiwa kumuua Jackline muda mfupi baada ya kutoka baa kulewa, tukio alilotenda Oktoba 4, 2020 eneo la Kimara Bucha nyumbani kwake.
Uamuzi huo umetolewa leo Jumatatu Julai 3, 2023 na Jaji John Nkwabi wa mahakama hiyo, baada ya mshtakiwa kutiwa hatiani kwa kosa la kuua bila kukusudia.
Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Judith Kyamba akishirikiana na Grace Mwanga, uliiomba mahakama hiyo itoe adhabu kali dhidi ya wakili huyo ili iwe fundisho kwa jamii.
"Mheshimiwa Jaji, pamoja na kwamba mshtakiwa ni mkosaji kwa mara ya kwanza na hatuna kumbukumbu za makosa ya nyuma, lakini kuna uhai wa mtu umetoka. Hivyo tunaomba apewe adhabu kali iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hii lakini pia adhabu hiyo iwe faraja kwa wafiwa," amedai Judith.