Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wakili kizimbani akidaiwa kuongoza genge la uhalifu

Muktasari:

  • Anadaiwa kuisababishia hasara ya Sh2.2 bilioni Wakala wa Ndege za Serikali.

Dar es Salaam. Wakili wa kujitegemea, Henry Kishaluli amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashtaka manne, likiwamo la kuongoza genge la uhalifu na kuisababishia hasara ya Sh2.2 bilioni Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA).

Kishaluli (51), amefikishwa mahakamani leo Desemba 20, 2023 na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Hemed Halfan, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Aaron Lyamuya.

Kabla ya kusomewa mashtaka, Hakimu Lyamuya amesema mshtakiwa hatakiwi kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Akimsomea mashtaka, Wakili Halfan amedai kati ya Oktoba mosi, 2011 na Machi mosi, 2014 katika Mkoa wa Dar es Salaam, mshtakiwa akishirikiana na wenzake tisa, kwa makusudi waliongoza genge la uhalifu kisha kusababisha hasara ya Sh2.16 bilioni kwa TGFA.

Shtaka la pili ni la kughushi nyaraka. Mei 28, 2013 mkoani Dar es Salaam mshtakiwa anadaiwa alighushi barua ya kumiliki akaunti ya benki kinyume cha sheria.

Akaunti inadaiwa kuwa na jina la Karim Hussein katika benki ya Habib African ikionyesha barua imeandikwa na kusainiwa na Karim Hussein jambo ambalo si kweli.

Inadaiwa Juni 3, 2013 katika benki ya Habib African wilayani Ilala mkoani Dar es Salaam, mshtakiwa aliwasilisha nyaraka hiyo kwa mkurugenzi mkuu wa benki hiyo.

Kishaluli pia anadaiwa kuisababishia TGFA hasara, ikidaiwa kati ya Oktoba mosi, 2011 na Machi 31, 2014 yeye na wenzake tisa kwa vitendo vyao waliusababishia wakala huo hasara ya Sh2.2 bilioni.

Upande wa mashtaka unadai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo umeiomba Mahakama kupanga tarehe kwa ajili ya shauri hilo kutajwa.

Hakimu Lyamuya aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 8, 2024, itakapotajwa na  mshtakiwa amepelekwa rumande.