Wakili wa Jacob 'Boni Yai', Malisa aeleza kinachoendelea polisi

Muktasari:

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linatarajia kuwahoji Boniface na Malisa leo Ijumaa

Dar es Salaam. Meya wa zamani wa Ubungo, Jacob Boniface maarufu Boni Yai na Mwanaharakati Godlisen Malisa wanatarajiwa kuanza kuhojiwa leo Ijumaa, Aprili 26, 2024 katika ofisi za upelelezi za Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kuhusiana na tuhuma zinazowakabili.

Wawili hao waliotiwa mbaroni jana Alhamisi, Aprili 25, 2024 walipokwenda kuripoti Kituo cha Kipolisi Mkoa wa Kinondoni Oysterbay, wakitii wito wa Kamanda wa Kanda hiyo, Jumanne Muliro wataanza kuhojiwa baada ya Jeshi la Polisi kukamilisha shughuli ya upekuaji kwenye nyumba ya Boniface na kuchukua simu waliyokuwa wanaitafuta.

kukosekana kwa simu wanazotumia kuchapisha taarifa zao kwenye mitandao ya kijamii ni sababu iliyosababisha wasihojiwe jana na Jeshi hilo.

Wakili wa wawili hao, Hekima Mwasipu amethibisha hilo wakati  akizungumza na Mwananchi Digital leo Ijumaa, Aprili 26, 2024 iliyokuwa inataka kujua hali ya watuhumiwa hao wa kosa la mtandao linalohusu pia kifungu namba 55 cha sheria  ya makosa ya jinai, uchochezi na kusababisha taharuki kwa jamii.

"Baada ya kumaliza upekuaji jana usiku kwenye nyumba ya Boniface na kufanikisha kupata simu wanaliyokuwa wanaitafuta, watuhumiwa wote sasa asubuhi hii wataenda moja kwa moja Ofisi za Kanda Maalumu kwa ajili ya kuanza kuhojiwa wakitokea Mbweni walikolazwa na Jeshi hilo," amesema Mwasipu

Mwasipu amesema mteja wake Malisa hajakwenda kupekuliwa Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro kama ilivyoelezwa jana na Jeshi la Polisi kwamba wangekwenda Moshi kupekua kwenye nyumba yake ili kupata simu huku akisema ratiba aliyonayo wawili hao wataanza kuhojiwa leo.

"Mahojiano yatafanyika leo, baada ya Jacob kupekuliwa ila Malisa hajapekuliwa," amesema Wakili Mwasipu

Boniface na Malisa wanatuhumiwa kuchapisha kwenye mitandao ya kijamii tuhuma kwamba Jeshi la Polisi lina ua raia. Kulingana na tuhuma hizo kwa mujibu wa Polisi zinachochea chuki kati ya jamii dhidi ya Jeshi la Polisi.

Wawili hao wanatuhumiwa kuchapisha taarifa kuhusu kupotea kwa Robert Mushi Dar es Salaam kisha mwili wake kupatikana katika mochwari ya Hospitali ya Rufaa ya Polisi Kilwa Road, jijini humo.

Mwili wa Mushi ulizikwa jana Alhamisi, Shirimatunda huko Moshi Mjini, Mkoa wa Kilimanjaro huku Boniface na Malisa wakidai kifo chake kimegubikwa utata.

Taarifa ya Polisi ilielezwa kuwa Mushi alifariki dunia kutokana na ajali.

Jitihada za kumpata Kamanda wa Polisi Kanda Maalum za Dar es Salaam, Jumanne Muliro zinaendelea kujua sababu za kutokwenda kumpekua Malisa na kinachoendelea kwa watuhumiwa hao.