Wakimbizi 12,000 waingia Tanzania ndani ya miezi sita

Mkurugenzi msaidizi wa Idara ya Wakimbizi, Kanishna Nsato Marijani akifafanua jambo kwa wahariri na waandishi mjini Morogoro leo Novemba 16, 2023.

Muktasari:

  • Tanzania ina zaidi ya wakimbizi 250,000 wanaoishi kambini na kwenye makazi maalum, ambapo asilimia 60 wanatokea nchini ya Burundi.

Morogoro. Mkurugenzi msaidizi wa Idara ya Wakimbizi, Kamishina wa Polisi Nsato Marijani amesema licha ya juhudi zinazofanywa na Serikali za kuwarudisha wakimbizi kwenye nchi wanazotoka, bado kuna wakimbizi wanaozidi kuwasili nchini, ambapo tangu Mei hadi Novemba zaidi ya wakimbizi 12,000 kutoka nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wameingia nchini na kusajiliwa.

 Ameyasema hayo leo Novemba 16 mjini Morogoro alipokuwa akizungumza na wahariri na waandishi wa habari katika warsha iliyoandaliwa na taasisi ya Dignity Kwanza, akieleza pia kuwa ufadhili unaotolewa na mashirika likiwemo Shirika la Umoja a Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) umepungua.

“Dunia inakabiliwa na majanga mengi, kuna Uviko-19, vita vya Ukraine na Russia na sasa vita vya Israel na Palestina, magonjwa na njaa, yote hayo yanasababisha kuwepo kwa wkaimbizi. Tangu Mei mwaka huu tumepokea zaidi a wkaimbizi 12,000 na bado wanaongezeka,” amesma.

Akizungumzia juhudi zilizofanywa na Serikali, Marijani amesema Serikali imekuwa ikiwarejesha kwa hiari baadhi ya wakimbizi na wengine wamepewa uraia.

“Katika makazi ya Nduta na Ulyankulu tumewarudisha kwa hiari zaidi ya wakimbizi 120,000, mwaka 1980 tuliwapa uraia wakimbizi 36,000, mwaka 1990 tuliwapa uraia wakimbizi 3,000, mwaka 2004 hadi 2010 pia tumewapa uraia wakimbizi wa Burundi 162,156 na wengine 46,000 tuliwapeleka nchi za Marekani, Canada na Australia.

“Tulidhani kwa kufanya hivi tutamaliza tatizo la wakimbizi, lakini bado wanaendelea kuingia,” amesema.

Awali akieleza chimbuko la wakibizi nchini, Profesa wa Sheria wa Shule kuu ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Khoti Kamanga amesema wakimbizi wa kwanza kuingia nchini, walikuwa ni Wapoland walioletwa na Waingereza kabla ya mwaka 1940 kufuatia vita vya kwanza vya dunia.

“Wakimbizi wengine kutoka Rwanda waiingia mwaka 1959 na wameendelea kuingia kwa nyakati tofauti,” amesema.

Mbali na wakimbizi, amesema dunia inakabiliwa na wimbi la wahamiaji na wakimbizi na biashara yausafirishaji wa binadamu, ambapo duiani kote kuna watu zaidi ya milioni 10 hawaa utaifa.

“Ili kupata suluhu ya kudumu, kwanza inatakiwa kuwarudisha majumbani kwao wale ambao sababu za kuishi kwenye ukimbizi hazipo, kuwatafutia nchi nyingine na kuwapa uraia,” amsema.