Chakula kwa waomba hifadhi kupunguzwa, wenyewe waiangukia Serikali

Kiongozi wa mradi wa ugawaji wa Chakula kwa wakimbizi katika kambi ya Nduta kutoka shirika la World Vision, Zakayo Kalebo akionesha unga wa mahindi kilo tano na nusu kwa mgao wa asilimia 50, ambao wanagawa kambini kwa mtu mmoja ndani ya mwezi mmoja.

What you need to know:

Hadi kufikia Mei, 2023 kambi za wakimbizi mkoani Kigoma zina wakimbizi 214,744 na kwamba toka Machi 5, 2023 hadi Mei 31, 2023 wamepokea waomba hifadhi 11,049 kutoka nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

kasulu. Wakimbizi wa kambi ya Nyarugusu na Nduta zilizopo mkoani Kigoma wamelalamikia kupunguziwa mgao wa chakula kutoka asilimia 65 hadi asilimia 50 wanaopokea kila mwezi ndani ya kambi hizo.

Akizungumza leo, Juni 8, 2023 kambini hapo mara baada ya kutembelewa na baadhi ya mabalozi wa nchi za Umoja wa Ulaya, Mwenyekiti wa kambi ya Nyarugusu upande wa warundi, Manirakiza Japhet amesema wamepokea taarifa ya kupunguziwa chakula kuanzia mwezi Julai mwaka huu kwa masikitiko na kuiomba Serikali ya Tanzania kuingilia kati suala hilo.

Japhet amesema taarifa hiyo ni changamoto kwao kama wakimbizi kwani sheria ya Tanzania haiwaruhusu kujishughulisha na shughuli zozote za kuwaingizia kipato nje ya kambi wala kufanya biashara ya aina yoyote ndani ya kambi.

“Tunaiomba Serikali ya Tanzania kuweza kuandaa mashamba kwaajili ya wakimbizi ili waweze kujishughulisha na masuala ya kilimo na kuweza kujikimu katika mahitaji yao,”amesema

Kiongozi wa mradi wa ugawaji chakula kwa wakimbizi katika kambi ya Nduta kutoka shirika la World Vision Tanzania, Zakayo Kalebo amesema awali walikuwa wanatoa asilimia 65 ambayo unga wa mahindi kilo kumi na nusu, maharage kilo tatu na nusu na mafuta ya kupikia nusu lita kwa mwezi kwa kila mtu mmoja kwenye kaya.

Kalebo amesema kwasasa watakuwa wanatoa asilimia 50 ya chakula ambacho ni kilo tano na nusu za unga wa mahindi, maharage kilo moja na nukta tisa pamoja na mafuta ya kula robo lita na kwamba hatua hiyo imekuja mara baada ya kupungua kwa fedha za uendeshaji wa huduma za chakula.

Mkurugenzi wa Idara ya Wakimbizi nchini Tanzania, Sudi Mwakibasi amesema suala la kupungua kwa chakula ni suala nyeti na la kiusalama akidai chakula kikipungua kuna athari ikiwemo kupungua kwa kiwango cha nidhamu kwa wakimbizi.

Mwakibasi ameiomba jumuiya ya kimataifa kuangalia namna ya kuboresha migao ya chakula ili isije ikawatoa wakimbizi kutoka katika hatua moja kwenda hatua nyingine ambayo si nzuri.

Mtaalam wa Lishe kutoka Shirika la Chakula Duniani (WFP), Sara Ruzangi amesema wamekuwa wakiona athari nyingi kwa wakimbizi kwa kutokupata chakula cha kutosha hasa kwenye makundi ambayo ni hatarishi kama watoto wa chini ya miaka mitano, wajawazito, kina mama wanaonyonyesha na watu wanaoishi na virusi vya ukimwi.

Msimamizi wa miradi kutoka WFP Wilaya ya Kibondo, Ali Ng’ombesazi amesema hatua hiyo ya kupungua kwa chakula kambini itasababisha kuzalisha wezi katika kambi hiyo, hasa watu wenye mahitaji maalum kuibiwa kutokana na hali zao.

Naye Mratibu Idara ya Wakimbizi Kanda ya Magharibi, Nashon Makundi amesema hadi kufikia Mei, 2023 kambi za wakimbizi zina jumla ya wakimbizi 214,744 na kwamba toka Machi 5,2023 hadi Mei 31, 2023 wamepokea waomba hifadhi 11,049 kutoka nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kutoka na machafuko yanayoendelea nchini mwao.

Amesema katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Mei 2023 jumla ya wakimbizi 1,343 kutoka familia 527 walirudi kwa hiari nchini kwao  Burundi.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa kambi ya Nyarugusu kwa upande wa wakongo, Asende Meshack amesema wanakabiliwa na changamoto ya nishati ya kupikia ndani ya kambi hiyo hivyo wanapendekeza kupewa gesi kwaajili ya matumizi yao ya kupikia kwa kila siku.

Amesema katika upande wa afya kambini hapo kumekuwa na changamoto ya upungufu wa watumishi wa afya na vitendea kazi ukilinganisha na idadi ya wakimbizi waliopo na kuomba utatuzi wa changamoto hiyo.