Wakulima 25, 000 kunufaika na mradi wa kilimo Tabora, Shiyanga

Mkurugenzi wa shirika la Small Enterprises Institutional Developmpent (SEIDA) Fredrick Ogenga akifafanua jinsi mradi wa kilimo utakavyofanya kazi Tabora na Shinyanga. Picha na Suzy Butondo

Muktasari:

Wakulima 25,000 wa halmashauri za Mkoa wa Shinyanga na Tabora wanatarajia kunufaika na mradi wa vijana kilimo biashara utakaowasaidia kulima mazao yanayostahimili ukame ikiwemo, alizeti, mtama mweupe na mbogamboga.

Shinyanga. Wakulima 25,000 wa halmashauri za Mkoa wa Shinyanga na Tabora wanatarajia kunufaika na mradi wa vijana kilimo biashara utakaowasaidia kulima mazao yanayostahimili ukame ikiwemo, alizeti, mtama mweupe na mbogamboga.
 
Halmashauri hizo ni Kishapu, Msalala, Shinyanga vijijini, Msalala, Ushetu, Nzega, Igunga, Uyui, Sikonge na Tabora Mji.
 
Akitambulisha mradi huo hivi karibuni kwa wataalamu wa kilimo wa halmashauri hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la SEIDA, Fredrick Ogenga amesema mradi huo unatekelezwa na shirika hilo kwa kushirikiana na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ambapo asilimia 70 ya wanawake watanufaika na vijana pia watanufaika kwa asilimia 70.
 
Ogenga amesema katika mradi huo ulioanza Oktoba mwaka huu na kutarajia kuisha Septemba 2026, wakulima hao watanufaika kwa miaka mitatu kwa kulima mazao makuu ambayo ni alizeti, mtama mweupe na mboga mboga.
 
Amesema malengo makubwa ya mradi huo ni pamoja na kuongeza kipato cha vijana na wanawake katika mikoa hiyo ambapo wazalishaji na wakulima wadogo watawezeshwa kuongeza kipato ili kufanya uzalish unaokidhi mahitaji ya soko, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha matumizi na upatikanaji wa mbegu bora.
 
“Mbegu bora zitapatikana kupitia wazalishaji wa daraja la mbegu za kuazimia (QDS) kwenye kata na vijijini ili kupunguza upotevu wa mazao wakati na baada ya mavuno na pia kupitia makundi ya watu wenye mahitaji maalumu na mwisho kuimarisha vyama na asasi za wazalishaji, wakulima kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa masoko na huduma za pembejeo,”amesema Ogenga

“Sifa za mkulima awe na miaka 18 na kuendelea, kipaumbele ni wanawake na vijana…tutachukua mtu  zaidi ya mmoja kwenye kaya, vijiji na kata ambazo zina vikundi na vyama vya msingi wa mazao, mifuko ya kuweka na kukopa na makundi ya vijana na wanawake ambayo yametambuliwa na idara za mamlaka za halmashauri husika katika maeneo yanayolima mazao hayo,”ameongeza
 
Amesema sababu nyingine kubwa ni soko la mtama mweupe kuwa la uhakika kwani WFP linahudumia nchi ya Sudan Kusini kwa msaada wa chakula na mahitaji ya mtama mweupe ambayo ndiyo chakula kikuu cha nchi hiyo ambayo inahitaji zaidi ya tani 200,000.
 
Ofisa kilimo wa Halmashauri ya Kishapu, Sabinus Chaula ameshukuru uwepo wa mradi huo akidai utasaidia kuongeza chakula kimkoa pamoja na kuwafanya wakulima kulima kilimo chenye tija ambacho kitaongeza kipato kutokana na kupatikana kwa soko la uhakika.