Wakulima Mbarali waeleza mafanikio ya kilimo shadidi

Baadhi ya wataalamu wa kilimo wakitembelea mashamba ya mpunga yaliyolimwa kwa kilimo shadidi.

Muktasari:

  • Mafunzo ya kilimo shadidi yaliyotolewa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) yamewavutia wakulima kutokana na ongezeko la mavuno waliyopata.

Mbarali. Wakulima wa mpunga wilayani Mbarali Mkoa wa Mbeya wameeleza mafanikio waliyopata kutokana na mbinu ya kilimo shadidi cha mpunga wakisema imewawezesha kuapata mafuno mengi zaidi.
Wakizungumza siku moja kabkla ya maadhimisho ya Nanenane Agosti 7 yaliyofanyikia katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, wakulima hao wanaounda skimu ya Kapunga wamesema Mafunzo waliyopewa a Shirika la chakula na kilimo la Umoja Mataifa (FAO) pamoja na Umoja wa Ulaya (EU) yaewawezesha kupata mavuno mengi.
“Kabla ya mradi wa shirika la FAO nimekuwa nikilima na kupata gunia kati ya 20 mpaka 22 kwa ekari lakini sasa hivi mafunzo tuliyopewa yameleta manufaa makubwa,” amesema mkulima wa kijiji cha Kapunga, Kata ya Itamboleo Baragasi.
Alisema mafuunzo waliyopewa na FAO yaliambatana na mbegu bora aina ya SARO 5 walipanda shamba darasa kwa kuchelewa lakini walipata magunia 38 katika ekari moja.
“Lile shamba langu ambalo nilikuwa nimepanda awali kwa kuwahi musimu, nilipata gunia 22 wakati shamba la kikundi ambalo tulipata mafunzo kutoka FAO tulipata gunia 38 kwa ekari,” amesema.
 Alisema tofauti na kilimo cha zamani, kilimo shadidi kupitia shamba darasa lao hawakutumia viuatilifu kuulia magugu, bali walitumia kifaa maalum kiitwacho ‘Push weeder’ na hivyo kuyalinda mazingira dhidi ya kemikali zenye sumu.
Naye Meshack Lyenje, Mkulima na Mkaazi wa kijiji cha Kapunga, Itamboleo alisema amekuwa akilima kwa zaidi ya miaka tisa na katika kipindi chote hicho amekuwa akipata chini ya gunia 30 kwa ekari moja.
“Kutokana na mafunzo haya, mwakani nategemea kulima ekari tano ambazo nitazitunza vizuri kwakuzingatia mafunzo niliyoyapata. Nategemea kupata gunia 190 kama kila ekari itatoa gunia 38,” alisema.
“Uzuri wa kilimo hiki huwezi kupata tabu kutumia dawa kwa sababu unatumia kipalizi ambacho unasukuma kwa mkono kwa kufuata vipimo vile ambayo mmepanda kwa mstari ulionyooka,” ameongeza.
Akizungumzia uzalishaji huo, ofisa mazao wa Wilaya ya Mbarali, Jamson Mwailana amewapongeza FAO na Umoja wa Ulaya kwa kuinua kilimo na kipato cha wakulima wanaotekeleza kilimo shadidi Wilayani humo.
“Kulingana na watalaam wanaotekeleza mradi huu na kipato cha wakulima wa kilimo shadidi ni dhahiri kuwa kumekuwa na mafanikio makubwa tofauti na kilimo cha mazoea cha hapo awali,” alisema.
Mratibu wa Mradi wa kuwajengea uwezo wakulima kutoka FAO, Diomedes Kalisa alisema mradi huo unatekelezwa katika nchi za Afrika, Caribbean na Pacific.
Kwa Afrika unatekelezwa Tanzania, Rwanda na Zimbabwe, na malengo yake makubwa ni kutumia mbinu nzuri za kiikolojia ili kuwa na kilimo endelevu, kulinda bionuai na kuongeza kipato kwa wakulima.
Amesema mradi huo unatekelezwa katika wilaya sita. Wilaya hizo ni pamoja na Mbarali, karatu, Same, Kilololo, Kigamboni na Kilosa.
“Katika Wilaya hizi tumefanya mashamba darasa nane ili kuwafundisha wakulima mbinu bora mbali mbali za kilimo,” anasema.
Alisema katika kilimo cha shadidi wakulima wanatunza bionuai kwa kutunza mazingira, kutumia maji kidogo ambayo pia yanasaidia kuwezesha uhai wa viumbe vya ardhini ambavyo havihitaji maji mengi.