Wakulima Rukwa wachekelea ahueni mbolea ya ruzuku, bei ya mazao ikipaa

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe (katikati) akiwafafanulia jambo baadhi ya wakulima wa mkoani Ruvuma aliowakuta katika ghala la kampuni ya ETG wakinunua mbolea ya ruzuku, mjini Sumbawanga, jana. Picha na Edwin Mjwahuzi

Rukwa. Wakulima wabainisha malalamiko kudai upatikanaji mbolea ya ruzuku ya kutosha katika maeneo mbalimbali nchini huku wakishangilia kupaa kwa bei ya mazao yao.

Wakulima wa mkoani Rukwa wameweka wazi kwa kusema kuna sababu kuu mbili ambazo ndio chanzo kikuu cha malalamiko hayo huku wakizitaja ni fedha wanazoendelea kuzipata kwa sasa wanapouza mazao yao na punguzo la bei ya mbolea kufuatia Serikali kuwezasha uuzwaji wa mbolea ya ruzuku.
Mkulima katika eneo la Mazwi, Josephat Mashauri amesema msimu wa kilimo wa mwaka 2020/2021 wakulima walipata hasara kubwa ambapo gunia la mahindi walikuwa wakiuza kati Sh20,000 hadi Sh30,000.
“Kusema kweli wakulima tumepata neema kubwa kwa kupata bei nzuri ya mahindi, kwa sasa hapa Sumbawanga tunauza gunila la mahindi kati ya Sh120,000 hadi Sh140,000.”

“Wakulima wengi baada ya kuona bei imepanda sana wengi wao wameongeza ukubwa wa mashamba yao na kusema ukweli msimu huu wa mwaka 2022/2023 tutazalisha mahindi mengi, tunaomba tu Serikali waendelee kufungua mipaka ili tufanye biashara na sisi tuchangie kuongeza pato la Taifa letu.” Alisema Josephat.

Wakulima wamemuomba Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe aliyefanya ziara mkoani humo awasaidie kupata mbolea ya kutosha katika maeneo yao kwani wamekuwa wakipata changamoto ya kusafiri umbali mrefu kuifuata mbolea mijini huku wao mashamba yao yako vijijini na wengine wanasafiri hadi umbali wa kilometa 150 hadi 200.

“Mheshimiwa Waziri (Bashe) wakulima tulilia sana bei ya mbolea ya msimu 2021 /2022 ilituumiza sana, sasa Serikali mmeonyesha mapenzi yenu kwa wakulima kwa kutupatia mbolea ya ruzuku hapa mjini ipo ya kutosha kwenye maghala tunaomba itufikie hadi vijijini kwetu ili kutuondoshea usumbufu sisi wakulima wa huko,” alisema mkulima Beda Chipanga.

Nae Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Aida Khenan amesema si utamaduni wake kupongeza ila anampongeza Waziri Bashe kwa kazi anayoifanya ya kusimamia wizara yake ikiwemo kupambana na kuondoa changamoto zinazowakabili wakulima.
“Ndugu yangu Waziri Bashe ile bei ya mwaka jana na ambayo ipo mpaka sasa sokoni ya gunia moja la mahindi kuuzwa Sh120, 000 imetia molali kubwa sana kwa wakulima kwa hiyo idadi ya watu kulima imeongezeka.”

“Mwaka jana mimi nililima eka mbili, mwaka huu nina ekari 38 kwa hiyo unaweza kuona mimi ni mmoja na mwenyekiti wangu wa halmashauri amelima ekari 100 sasa hatujui huko kwengine wakulima wameongeza kilimo kwa ukubwa gani.” Alisema Aida

“Swala la kuitaka Serikali kuweka ruzuku kwenye mbolea nalo pia limeongeza molali sana kwa wakulima, kwa hiyo tuombe pamoja na nia njema ambayo imeshafanyika yakuweka ruzuku basi mbolea ifike kwa wakati.”

Waziri Bashe amesema mbolea ipo na katika ziara alipotembelea maghala kadhaa mjini Sumbawanga ameikuta, ila amekili kuwepo changamoto ya usambazaji wake kufika vijijini.

“Hii ni kazi ambayo tunatakiwa tuifanye kwa pamoja, nimeitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kila mkoa awepo mtu mmoja na kila wilaya kuwepo afisa anayeshughulikia mbolea ili mzigo wa mbolea unapoisha kwa msambazaji kuwe na taarifa.”

Bashe amesema jambo kubwa aliloliona katika ziara yake mkoani humo ni ongezeko la mahitaji ya mbole kwa wakulima tofauti na msimu wa kilimo uliopita.

“Tumetembelea kampuni ya usambazaji wa mbolea ya ruzuku ya OCP ghala lao kwa msimu wa kilimo mwaka 2021/2022 waliuza katika Mkoa wa Rukwa tani 1120, lakini mpaka leo msimu mpya wameshauza zaidi ya tani 4200.”

“Wilaya ya Nkasi kwa mwaka mzima msimu wa kilimo uliopita walitumia tani 1600, mpaka sasa Serikali imepeleka tani 842 kwa hiyo ni zaidi ya asilimia 50 ya maitaji ya mwaka uliopita.” Alisema Bashe.

Bashe amesema wakulima wengi wameongeza maeneo ya kilimo na mashamba yao huku wakiwa wameonyesha utayari wa kulima sana kwa sababu ya kuvutiwa na soko la bidhaa zao.