Wakulima  wa Kakao mkoani Mbeya wapewa mbinu mpya kulikamata soko

Zao la Kakao likiwa shambani

Muktasari:

  • Wakulima wa Kakao mkoa wa Mbeya wametakiwa kujiunga kwenye vikundi vya ushirika ili kuwa na sauti moja itakayowasaidia kuamua bei nzuri ya kuuza zao hilo sokoni.

Mbeya. Wakulima wa zao la Kakao mkoani Mbeya wametakiwa kuacha kutengeneza matabaka na badala yake waungane kupitia vyama vya ushirika ili kuwa na sauti moja itakayo wawezesha kuamua bei nzuri itakayo wanufaisha  wanapohitaji kuuza bidhaa hiyo sokoni.

Ushauri huo ulitolewa leo Mei 26, 2023  wilayani Kyela na Kaimu Meneja Mkuu wa Ushirika (Kyecu), Julius  Mwankenja anayedai kuna baadhi ya wakulima wanauwezo wa kufanya maamuzi lakini wamekuwa wakijitenga na wenzao hali inayowarudisha nyuma.

"Wakulima wakiungana wanakuwa na nguvu tumeona safari hii, licha ya wakulima wengi kuuza bidhaa hiyo kwa mfumo wa stakabadhi ghalani kupitia ushirika lakini hawashiriki kwenye maamuzi ya bei kwakuwa siyo wanachama," amesema.

Julius amesema Ili mkulima uweze kushiriki maamuzi ya kuamua bei kwenye minada wanayofanya kila wiki, nilazima awe mwanachama hai kwenye vikundi vya msingi vya ushirika.

"Tunaona wakulima wengi wanauwezo wa kufanya maamuzi mazuri yatakayoleta tija kwao lakini hawapati fursa hiyo kwakukosa sifa," amesema.

Hoja iliyoungwa mkono na Afisa Ushirika Wilaya ya Kyela, Thadei Mwambeso anayedai kwa sasa serikali inawasikiliza wakulima na kutoa fursa tofauti kwao kupitia Vyama vya ushirika.

"Serikali ikitaka kutoa pembejeo bora na kwa bei na fuu wanaanza kupitia kwenye vyama vya ushirika hadi wakinufaika wale ndipo wanaanza kuangalia wengine ni muhimu kujiunga," amesema.

Amesema kupitia mfumo huo mazao ya wakulima yanauzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani ambapo ndani ya saa 24 mkulima anaanza kupata malipo yake kupitia simu yake.

"Katika mfumo wa stakabadhi ghalani hakuna watu kunyonywa na hata vipimo vinavyotumika ni vya kidigijitali hata pointi chache za mkulima zikibaki anaziona," amesema

Mkulima wa zao hilo Bruno Benedict amesema kudanganywa na baadhi ya wafanyabiashara ni moja ya sababu zinazochelewesha wakulima wengi kusita kujiunga na vyama vya ushirika.

"Wamekuwa wakidanganywa lakini tunaomba Mamlaka kuzidi kutoa elimu kwa wakulima kwani jambo lolote linapoanzishwa hakukosekani watu wanaopinga siyo wakati wa kurudi nyuma tunatakiwa kusonga mbele," amesema.