Wakulima wa pamba waongezeka Bukombe

Muktasari:

Wakulima wa zao la pamba wameongezeka kutoka 8, 000 mwaka jana kufikia 11, 000 mwaka huu Wilaya ya Bukombe mkoani Geita.

Bukombe. Wakulima wa zao la pamba wameongezeka kutoka 8, 000 mwaka jana kufikia 11, 000 mwaka huu Wilaya ya Bukombe mkoani Geita.

Akitoa taarifa ya uzalishaji wa zao hilo na changamoto zilizojitokeza Mei 31, 2023, Ofisa Mkaguzi Bodi ya  Pamba Wilaya  ya Bukombe, Jemes Edmond amesema kutokana na ongezeko hilo la wakulima msimu huu wanatarajia kuvuna kilo 4 milioni kwa vile hata hali ya hewa ni nzuri.

“kwa mwaka jana Wilaya ya Bukombe tulitarajia kuvuna pamba  kilo 3.8 milioni lakini kushuka kwa uzalishaji tulivuna kilo1.8 milioni,”

“Uzalishaji ulishuka kwa sababu ya kubadilika hali ya hewa, kuwaka jua kali ambapo kwa msimu huu hali hiyo haikujitokeza hivyo tunatarajia kuvuna pamba nyingi,” amesema Edmond

Ametaja mikakati ya Serikali wilayani humo ni kuendelea kupandisha uzalishaji wa zao hilo kwa kusambaza  pembejeo za kilimo zikiwemo mbegu na dawa za kuuwa wadudu  kwa wakati.

Amesema kulingana na changamoto  iliyotokea mwaka jana, Serikali imewafutia madeni ya pembejeo wakulima yakiwemo madeni ya  mbegu za pamba tani 296, vinyunyuzi 550, dawa za kuuwa wadudu chupa 312,784 na pembejeo yote yakigharimu Sh1.9 bilioni.

“Serikali imesamehe huku ikiwataka  wauze bei elekezi ya Sh1,600 kwa kilo moja bila makato ya pembejeo tofauti na hapo kampuni inunue bei ya juu, ”amesema

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Paul Cheyo ameviomba Vyama vya Msingi kushirikiana na makampuni ya ununuzi wa pamba vizuri kwa kuacha kuwakopa wakulima badala yake ziwalipe kwa wakati ili Wasitoroshe pamba.

"Nawaombeni sana vyama vya msingi ambavyo mmepewa dhamana ya kisheria kusimamia wahasibu wasikope pamba ili wakulima wasitoroshe pamba kwenda kituo kingine au nje ya Wilaya na makampuni yashindane kwa bei elekezi kwa kuongeza bei ili Serikali ipate mapato mengi na wakulima wakuze uchumi wa familia zao,"amesema Cheyo

Ofisa Kilimo Kata ya Bugelenga, Sadick Kamishe amesema kichocheo kikubwa cha mkulima kutorosha pamba ni mhasibu na kampuni husika kukosa fedha na kutaka kukopa pamba kwao.

"Wakulima  wanafuata fedha hawataki kukopwa ndomana Wanatorosha pamba kutoka eneo walilo pangiwa kuuzia wanaenda maeneo ya jirani muda mwingine wanalazimika kwenda nje ya wilaya kwenye bei nzuri, ”amesema

Mkulima wa zao la pamba kijiji cha Kiziba, Charles Yohana amesema mwaka huu amepata pamba kutokana na kupewa pembejeo kwa wakati huku, Emmanuel Stephano mkulima wa pamba kijiji cha Bwenda ameiomba Serikaki kuendelea kusambaza pembejeo kwa wakati ili wakulima wafikie malengo yao.