Wakulima wa parachichi wafundwa kilimo bora

Mtaalamu wa kilimo kutoka Taasisi ya Mbogamboga na Matunda (Taha) akiwaonesha wakulima wa parachichi Wilaya ya Iringa namna ya kupunguza matawi ya mti aliobaini umepata ugonjwa.

Muktasari:

  •  Iringa ni kati ya mikoa inayolima parachichi kwa wingi licha ya kuwa baadhi ya wakulima hawajui mbinu za kilimo bora na namna ya kuufikia ubora unaotakiwa kwenye soko la kimataifa.

Iringa. Wakulima wa parachichi Wilaya ya Iringa mkoani hapa, wamemuita mtaalamu wa kilimo shambani ili awasaidie ujuzi wa kilimo, namna ya kupambana na magonjwa ili kufikia ubora wa soko la kimataifa.

Iringa ni kati ya mikoa inayolima parachichi kwa wingi licha ya kuwa baadhi ya wakulima, hawajui mbinu za kilimo bora na namna ya kuufikia ubora unaotakiwa kwenye soko la kimataifa.

Mtaalamu wa kilimo cha zao hilo kutoka Taasisi ya Mbogamboga na Matunda (Taha) Steven Tumaini amesema imekuwa rahisi kuitika wito na kuwafikia wakulima  baada ya kuwa wamejiunga kwenye kikundi.

Akizungumza na Mwananchi leo Aprili 22, 2024, Mwenyekiti wa wakulima wa parachichi Wilaya ya Iringa, Wiles Nyaulile amesema lengo lao ni kuhakikisha kilimo hicho kinainua uchumi wao.

"Ni kundi ambalo tumeunda hivi karibuni na tulitaka kulifikia soko kwa pamoja, tulipoona kuna maswali mengi kuhusu parachichi ilibidi kwa pamoja tumuite mtaalamu," amesema Nyaulile na kuongeza;

"Tatizo la kilimo hiki usipojua mbinu na namna ya kuzalisha parachichi bora hupati soko, parachichi zinaharibika na utajikuta zinakataliwa sokoni."

Steven amesema soko la uhakika la zao hilo ni kubwa kuwa jambo la msingi kwa wakulima ni kufuata mbinu za kilimo Ili kulinda ubora.

"Wakulima hawa wameniita na hatujakaa darasani, tumetumia muda wote shambani, changamoto nilizokutana nazo, nimewaonyesha jinsia ya kutatua ikiwamo kukata matawi ya miti," amesema.

Amesema jambo la msingi kwa mkulima wa parachichi ni kuhakikisha shamba lake lina maji ya kutosha na mbolea ya uhakika ya samadi ili kurutubisha udongo.

Mbali na elimu hiyo, amewaunganisha na masomo ya parachichi ambapo wanunuzi hufuata mazao shambani.

Baada ya kustaafu utumishi wa umma, Nyaulile na mke wake Argentina Kibassa wamelima shamba lenye ukubwa wa eka 10 na  kufanikiwa kuvuna Sh18 milioni tangu walipoanza kuvuna miaka miwili iliyopita.

Mkulima mwingine wa parachichi, Exaud Sanga amesema changamoto iliyokuwa inajitokeza kwenye shamba lake ni majani kujifunga.

"Nimeelewa na nitatatua changamoto shambani kwangu,shida yangu ilikuwa ni majani kujifunga juu," amesema.