wakulima wapewa 'mchongo'
Muktasari:
- Wakulima nchini wameshauriwa kutumia fursa kutoka taasisi za kilimo na benki ili kuboresha sekta ya kilimo.
Dar es Salaam. Wakulima nchini wameshauriwa kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na taasisi za kilimo pamoja na kibenki kwa lengo la kuwawezesha kukuza mnyororo wa thamani katika sekta na hatimaye kuchangia pato la taifa.
Haya yameelezwa mkoani Dodoma katika maonesho Nane Nane na wadau wa fedha na kilimo wakati Naibu Waziri wa Kilimo, Davis Silinde akishuhudia utiaji saini mkataba wa mashirikiano MOU kati ya taasisi tatu ambozi ni Benki ya Equity, Taasisi ya Biashara ya PASS na Taasisi ya MCODE zenye lengo la kuboresha maisha ya Watanzania hasa wakulima.
Akizungumza mara baada ya utiaji saini makubaliano hayo na Meneja Mkuu wa Biashara wa Benki ya Equity, Leah Ayoub amesema mkataba huo una lengo la kuboresha maisha ya wakulima walioko vijijini wanaohitaji kupata huduma za kifedha hususani mikopo lakini hawana dhamana za kupata mikopo.
Leah amesema makubaliano hayo yawawia wakulima urahisi wa kupata dhamana za mikopo pasipo gharama yeyote.
Naye Mkurugenzi wa Biashara kutoka taasisi ya PASS, Adam Kamanda ameeleza kuwa mikataba hiyo ni kwa ajili ya uendelevu kibiashara ambapo watawasaidia wakulima kulima kisasa ,ili kuongeza tija katika mazao yao na kukuza mnyororo wa thamani kwenye sekta ya kilimo, ambapo mpaka sasa wamefikiwa wakulima elfu 30 na lengo ni kufikia watu zaidi ya laki moja.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya MCODE, Slaiton Kaberege amesema kuwa pamoja na hayo pia wanawezesha wakulima kupata pembejeo, na mpaka sasa wamekwisha kupata mikopo yenye thamani ya Sh20 bilioni wakiwa na vikundi 1,000 kwenye mikoa sita.
“Benki ya Equity inaamini kupitia uwezeshaji wa wakulima wadogo wadogo walio katika vikundi kutaiwezesha benki hiyo kufikisha huduma za kifedha kwa wananchi wengi zaidi hivyo kutimiza lengo la serikali ya kuboresha sekta ya kilimo ambayo imeajiri watu wengi na yenye mchango mkubwa zaidi katika pato la taifa.”
“Ni dhamira ya Benki ya Equity kufanya kazi na wadau wote wenye malengo na maono yanayoendana na Serikali katika kuhakikisha inachangia juhudi za serikali kwenye sekta ya kilimo hasa hasa Agenda 2030.” Amesema Kaberege.