Wakulima wapewa somo kufaidi korosho

Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari Naliendele) Dk Furtunus Kapinga (aliyesimama mbele) akielekeza namna bora ya kupanda mche wa korosho. Picha na Florence Sanawa

Muktasari:

Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari Naliendele) Dk Furtunus Kapinga amewaonya wakulima wa korosho kuacha kupalilia mashamba wakati wa kiangazi badala yake waanze kupalilia wakati mvua zinanyesha.

Mtwara. Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari Naliendele) Dk Furtunus Kapinga amewaonya wakulima wa korosho kuacha kupalilia mashamba wakati wa kiangazi badala yake waanze kupalilia wakati mvua zinanyesha.

Dk Kapinga ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Desemba 13, 2021 alipotembelewa na Umoja wa Wanawake wa  Kanisa la Anglican Mtakatifu Gabliel wa Mikoa ya Pwani na Mtwara ambapo alisema kuwa ili kupata mavuno mengi yenye tija mkulima anapaswa kufuata maelekezo yanayotolewa na watalaamu zao hilo.

"Wapo wakulima hawapalilii kwa kulima bali wanakwangua majani tu ni vema mkulima anapaswa apalilie kwa jembe au trekta kwa mwezi huu wa Desemba mpaka Januari”

"Wakulima sasa hiyo ndio kazi kubwa waliyonayo kwakuwa mkorosho unajiandaa kuchipua hivyo unapaswa kupaliliwa wakati huu ili virutubisho vinavyotoka ardhini viingie kwenye matawi yenye tija yatakayoleta manufaa kwa mkulima" amesema

Naye Josephina Mhina kutoka Mkoa wa Pwani amesema kuwa zao la korosho linahitaji mafunzo ya kila mara ili kumuwezesha mkulima kufanya kilimo chenye tija.

"Nimejifunza kilimo cha korosho najiandaa nimevutiwa kulima zao la korosho nitarudi tena katika kituo hiki kujifunza zaidi wakati mwingine tunasikia mitaani jinsi kilivyokigumu hadi tunaopa lakini nafikiri ni elimu tu bado haijatufikia ipasavyo" alisema Mhina