Walemavu wa miguu 130 kunufaika na vifaa saidizi
Wanachama wa Club mbili za mazoezi ya kukimbia Jogging za jijini Tanga, Tanga Raha na OTABI wakiwa kwenye mazoezi ya kuunga mkonmo mpango wa kugawa miguu bandia na viti mwendo kwa watu wenye mahitaji maalumu Julai 14, 2026. Picha na Mbonea Herman.
Muktasari:
- Ugawaji wa vifaa hivyo utafanyika Julai 14, 2026 na utaambatana na mafunzo kwa walengwa na washiriki wengine kuhusu namna ya kutumia fursa zinazotolewa kupitia asilimia 30 ya zabuni za manunuzi ya umma zinazotengwa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Tanga. Walemavu wa viungo 100 kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Tanga wanatarajiwa kunufaika na miguu bandia, hatua inayolenga kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji, kujipatia kipato na kuboresha maisha yao.
Mbali na miguu hiyo, watu wengine 30 wenye mahitaji maalumu watanufaika na viti mwendo pamoja na fimbo za kutembelea zitakazowasaidia wazee na watu wenye changamoto za kutembea.
Ugawaji wa vifaa hivyo utafanyika Julai 14, 2026 na utaambatana na mafunzo kwa walengwa na washiriki wengine kuhusu namna ya kutumia fursa zinazotolewa kupitia asilimia 30 ya zabuni za manunuzi ya umma zinazotengwa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Akizungumza leo Jumapili, Julai 12, 2026 wakati wa kuhitimisha mazoezi ya kukimbia yaliyoandaliwa na klabu za Tanga Raha na Otabi, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga (CCM), Mwanaisha Ulenge amesema mafunzo hayo yanalenga kuongeza uelewa kwa watu wenye mahitaji maalumu kuhusu fursa zilizopo ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Amesema bado wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu Sheria ya Manunuzi ya Umma na fursa ya asilimia 30 ya zabuni zinazotengwa kwa makundi hayo.
"Kwa mfano, bajeti ya mwaka huu ni takribani Sh62 trilioni, ambapo zaidi ya asilimia 80 ya fedha hizo huenda kwenye manunuzi ya umma. Hivyo, asilimia 30 ya manunuzi hayo inapaswa kunufaisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Changamoto ni kwamba ni wachache wanaofahamu na kutumia fursa hizo," amesema Ulenge.
Amesema kuambatanisha mafunzo na ugawaji wa vifaa saidizi kutasaidia kuwajengea uwezo walengwa na kuwahamasisha kutumia fursa zinazotolewa na Serikali.
Ulenge amesema mpango huo ni sehemu ya kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2020/2050 kwa kuwawezesha watu wenye mahitaji maalumu kuwa na uwezo wa kushiriki katika shughuli za kiuchumi baada ya kupata vifaa vitakavyorahisisha maisha yao ya kila siku.
Kwa upande wake, Mbunge wa Watu Wenye Ulemavu, Nasiria Nasiri amesema mpango huo utakuwa na mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu ambao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za kushiriki shughuli za kiuchumi kutokana na ukosefu wa vifaa saidizi.
"Nimefunga safari kutoka Zanzibar kuja kushiriki tukio hili kwa sababu linanigusa moja kwa moja. Nampongeza Mwanaisha Ulenge kwa moyo wa kujitolea kuwasaidia watu wenye ulemavu," amesema Nasiri.
Mwenyekiti wa Otabi Jogging and Fitness Club, Juma Omari amesema klabu hiyo imeamua kushiriki katika zoezi hilo kuunga mkono juhudi za kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu.
Amesema vifaa hivyo vitawapa walemavu wa viungo nafasi ya kushiriki kwa uhuru zaidi katika shughuli za uzalishaji na kujitegemea.
"Sisi tunaweza kukimbia na kufanya mazoezi, lakini wenzetu wengi hawawezi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kila siku kutokana na changamoto za ulemavu. Tunaamini vifaa hivi vitabadilisha maisha yao," amesema Omari.
Naye Mwenyekiti wa Tanga Raha, Hassan Nasri amewataka wadau mbalimbali kuendelea kuunga mkono juhudi za kuwapatia vifaa saidizi watu wenye mahitaji maalumu, akisema hatua hiyo inawapa fursa ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.