Walimu 250 wapewa mbinu kuepuka mikopo umiza

Muktasari:
Benki ya NMB imewakutanisha walimu zaidi ya 250 mkoani Mara katika kongamano la ‘walimu spesho’ lenye lengo la kutoa elimu ya kifedha ili kupata suluhisho la changamoto za kifedha wanazokumbana nazo likiwemo suala la mikopo umiza.
Musoma. Zaidi ya walimu 250 wa Mkoani Mara wamefundwa masuala ya kifedha ambayo yatawawezesha kujua namna ya kupangilia vipato vyao viendane na matumizi yao ili kuepuka kuchukua mikopo umiza katika taasisi zisizokuwa rasmi.
Mafunzo hayo yametolewa mjini Musoma Septemba 11, 2023 na benki ya NMB kwenye kongamano la walimu maarufu kama mwalimu spesho day.
Mkuu wa Idara ya Wateja Binafsi kutoka NMB, Aikansia Muro amesema mbali na mafunzo hayo lakini pia benki hiyo imekuwa ikibuni huduma mbalimbali rafiki kwaajili ya walimu ambao ni mojawapo ya kundi kubwa la wateja wao.
“Tunatambua umuhimu wa walimu, pia tunatambua changamoto kubwa wanayokutana nayo ambayo ni pamoja na hii mikopo umiza hivyo kutokana na umuhimu wa kundi hili sisi hatuwezi kuwaacha waendelee kuumia,”amesema
Amesema kutokana na hali hiyo benki hiyo imekuwa ikianzisha huduma mbalimbali ikiwepo mikopo maalum yenye masharti nafuu kwa kundi hilo ikiwa ni nia mojawapo ya kuwawezesha walimu kujiimarisha kiuchumi.
Akifungua kongamano hilo, kaimu Ofisa Elimu Mkoa wa Mara, Makwasa Bulenga amesema mikopo umiza ni moja ya changamoto inayokwamisha utoaji wa elimu kwa ufasaha mkoani Mara.
“Wakishakopa mikopo umiza hata ufundishaji unakuwa wa chini kwasababu wanakuwa na msongo wa mawazo yaani kwa ujumla mikopo umiza inasababisha utendajikazi wa walimu kushuka,”amesema
Bulenga amewataka walimu kutumia taasisi rasmi za kifedha kwajili ya kujipatia huduma za kifedha ikiwemo mikopo ili kuepuka changamoto wanazokutana nazo kwenye mikopo umiza hatua ambayo pia itawasaidia kujiimarisha zaidi kiuchumi.
Baadhi ya walimu wamesema uwepo wa huduma zenye masharti nafuu ni mkombozi wa walimu hasa kwenye suala zima la mikopo umiza.
"Sote tunajua waathirika wakubwa wa mikopo hiyo ya mitaani ni walimu, na walimu wengi wanafanya hivyo kutokana na masharti magumu yaliyopo kwenye taasisi za kifedha lakini kwasbabu kuna huduma maalum kutoka NMB naamini wengi tumepata suluhisho,"amesema Mwalimu Sophia John
Mwalimu Rosemary Kisenga ameishukuru benki hiyo kwa kuanzisha huduma rafiki kwao na kuzitaka taasisi zingine kuiga mfano huo hatua ambayo amedai itatokomeza mikopo umiza nchini kwani walimu wengi wataweza kukopa katika taasisi rasmi za kifedha.
"Kuna mikopo ya elimu, biashara na hata mikopo ya vyombo vya usafiri maalum kabisa kwaajili ya walimu hii ina maana kuwa benki hii imetambua maumivu ambayo walimu tunakutana nayo hivyo kuamua kuja na suluhisho la kudumu,”amesema