Walimu mbaroni wakidaiwa kughushi nyaraka za mikopo
![](/resource/image/4372750/landscape_ratio2x1/320/160/44ef0e13b9aa0702a136179edddceef7/OO/polisi-pic.jpg)
Muktasari:
- Jeshi la Polisi mkoani Mara linawashikilia watu 11 wakiwemo walimu sita wa shule za misingi za Mkoa wa Mwanza kwa tuhuma za kupatikana na nyaraka za kughushi walizotaka kutumia kwaajili ya kujipatia mikopo.
Musoma. Jeshi la Polisi mkoani Mara linawashikilia watu 11 wakiwemo walimu sita wa shule za msingi za Mkoa wa Mwanza kwa tuhuma za kupatikana na nyaraka za kughushi walizotaka kutumia kwaajili ya kujipatia mikopo.
Watu hao wamekamatwa kati ya Septemba 14 hadi 17 2023 katika maeneo tofauti ikiwemo Musoma na Mwanza wakiwa kwenye harakati za kujipatia mikopo kwa nyaraka hizo zinazodaiwa kughushiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Musoma leo Jumatatu Septemba 18, 2023, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Salim Morcase amesema watu hao walikuwa wakijiandaa kuchukua mikopo katika Chama cha Ushirika cha Chogo Credit cha mjini Musoma.
“Nyaraka walizoghushi ni pamoja na vitambulisho feki vikionyesha kuwa wao ni walimu katika halmashauri ya Manispaa ya Musoma, hati feki za mishahara (salary slip), taarifa za benki (bank statements) na vitu vingine,”amesema.
Amewataja walimu waliokamatwa kuwa ni pamoja na Pascal Mjinja (44), Meryciana Nyekia (50), Katambi Masudi (59), Halima Msuya (31), Getruda Boniface (36) na Aisha Nakala (36) wote walimu wa shule za Misingi mkoani Mwanza.
Wengine waliokamatwa wakituhumiwa kwa makosa mbalimbali ni pamoja na Martin Musira (63) mkazi wa Musoma, James Sebastian (64), Innocent Ndesabura (36), Gertrude Kokuberwa (47) na Samason Kabingili (59) wote wakazi wa Mwanza.
Amefafanua katika upekuzi wao wamekamata kompyuta, scanner na printa zilizokuwa zikitumika kutengengeza nyaraka hizo.
“Watuhumiwa Sebastian, Ndesabura na Musira wamekamatwa wakiwa na kompyuta tatu, printa mbili na scanner walizokuwa wakitumia kutengeneza hizo nyaraka feki pamoja na simu ambayo ilikuwa na oda za nyaraka zilizotakiwa kutengenezwa,”amesema
Kamanda Morcase ameongeza baada ya watuhumiwa kufika katika ofisi za chama hicho cha ushirika na kujitambulisha kama watumishi wa idara ya elimu katika Manispaa ya Musoma, wafanyakazi wa chama hicho waliwatilia mashaka na kutoa taarifa polisi.
Amesema uchunguzi unaendelea ili kubaini kama kuna mtandao zaidi wa watu wengine wanaojihusisha na watuhumiwa hao ili kujua kama wamekwishajipatia mikopo kwa njia hizo za udanganyifu ama wanapanga kufanya hivyo.