Walimu Mkoa wa Rukwa wadai Sh2 bilioni

Muktasari:

  • Kukithiri kwa malalamiko ya walimu kutolipwa stahiki zao mbalimbali kwa wakati, imetajwa ni miongoni mwa sababu zinazofanya walimu wengi kutotimiza majukumu yao kwa ufanisi pindi wawapo kwenye vituo vyao vya kazi.

Rukwa. Kukithiri kwa malalamiko ya walimu kutolipwa stahiki zao mbalimbali kwa wakati, imetajwa ni miongoni mwa sababu zinazofanya walimu wengi kutotimiza majukumu yao kwa ufanisi pindi wawapo kwenye vituo vyao vya kazi.

  

Kaimu Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mkoa wa Rukwa, Mrisho Kikonda amesema leo Januari 17, 2023 wakati akizungumza na Mwananchi ofisini kwake ambapo alitakiwa kueleza ni namna gani CWT inapambana kushughulikia madai ya walimu wa mkoa huo.

Kikonda pamoja na kukiri kwamba serikali imekuwa ikilipa stahiki za walimu hao lakini bado deni ni kubwa kiasi kwamba linasababisha manung'uniko na vinyongo kutoka kwa baadhi ya walimu hali inayofanya baadhi yao kutofanya kazi kwa moyo.

Amesema walimu wa mkoa huo, wanadai zaidi ya Sh Bilioni 2 ikiwa ni madai ya uhamisho, mishahara  matibabu, masomo, likizo na madai ya wastaafu.

"Kweli walimu wanavunjika moyo wa kazi pindi wanapoona madai yao hayalipwi kwa wakati...lakini niwaombe waendelee kufanya kazi kwa weledi mkubwa sisi (CWT) tunaendelea kuikumbusha serikali ili ione umuhimu  wa kulipa madai hayo kwa wakati" amesisitiza Katibu huyo.

Naye, Katibu wa CWT Wilaya ya Sumbawanga, Peter Simwanza amesema kuna wilaya, mathalani Sumbawanga vijijini ni vigumu kujua madai hali ya walimu kwa kuwa mwajiri hayuko tayari kufanya uhakiki wa madai hayo.

Amesema pia wakurugenzi ambao ndio waajiri hawataki kukaa vikao vya mabaraza ya wafanyakazi ambayo ndio yangekuwa chachu ya kujadili changamoto wanazokutana nazo walimu na ufumbuzi wake.

Ameshauri wakurugenzi kuacha tabia ya kukwepa kuitisha vikao hivyo kwa kuwa vipo kwa mujibu wa sheria za nchi.

Hivi karibuni baadhi ya walimu wakitoa maoni yao kwenye kikao cha wadau elimu wa mkoa huo kilichofanyika kwenye shule ya Sekondari ya Sumbawanga mjini hapa walidai walimu wengi vijijini hawana furaha ya kazi kwa kuwa serikali imeshindwa kulipa madai yao kwa muda mrefu sasa.

"Kilio cha walimu huko vijijini ni madai ya mapunjo ya mishahara "area's " kukosa fedha hizo kunafanya wafanye kazi kwa kinyongo," amesema Mwalimu Safu Ngonya ambaye ni Mkuu Shule ya Msingi Msanda Muungano.

Kupitia kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Queen Sendiga amewataka wakurugenzi wa halmashauri za wilaya kuhakikisha wanatatua kero za walimu ikiwemo kulipa madai yao mbalimbali ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kukuza kiwango cha elimu.

Aidha, kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi mkoa huo kimeshuka kutoka 80.15% kwa mwaka 2021 hadi 77.9 mwaka 2022, ambapo katika mtihani wa darasa la nne kiwango cha ufaulu kimeshuka kutoka 79.95% hadi 75.6%.

Na katika matokeo ya kidato cha pili mkoa umeshuka kutoka asilimia 92.0 hadi asilimia 63.3 huku kidato cha ukishuka kutoka asilimia 99.7 hadi 99.6 asilimia kwa mwaka 2022.