Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waliobiwa mtoto wa siku 42 wasimulia mkasa mzima

Mtoto wa siku 42 aliyeibwa.

Muktasari:

  • Mtoto huyo aliibwa katika Hospitali ya Nguvu Kazi Chanika alipopelekwa kwa ajili ya kupata chanjo.

Dar es Salaam. Wazazi waliobiwa mtoto wao mwenye umri wa siku 42, wameeleza mkasa mzima ulivyokuwa kabla na baada ya kutokea kwa tukio hilo.

Wazazi hao ambao ni wakazi wa Chanika Masantula, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, mtoto wao huyo aliibwa katika hospitali ya Nguvu Kazi  iliyopo Chanika wilayani humo walipokuwa wamepeleka kwa ajili ya kupata chanjo.

Kamanda wa Kanda Maalum mkoa wa  Dar es Salaam, Jumanne Muliro amekiri kupokea taarifa hiyo na kueleza kuwa wanalifuatilia tukio hilo kwa ukaribu.

Wakisimulia kwa nyakati tofauti, walipozungumza na Mwananchi Digital iliyofika nyumbani kwao Chanika, mama wa mtoto huyo, Sharifa Kassim, amesema ilikuwa Julai 6,2026  majira ya saa 1:30 asubuhi  alipofika hospitalini hapo kwa ajili ya kumchoma mtoto wake huyo chanjo ya kwenye mapaja.

Sharifa amesema akiwa hapo alifanikiwa kuanza kupata huduma nyingine ikiwemo kufungua kadi kusubiri kupata huduma ya mtoto kuchomwa sindano.

Hata hivyo, kutokana na kuwepo kwa foleni ndefu alikuwa amekaa kwenye viti akisubiri zamu yake ifike lakini akiwa bado hapo kwenye majira ya saa tano mtoto akajisaidia hivyo akawa anamsafisha.

Wazazi wa mtoto aliyeibwa.

Wakati akiwa anafanya hivyo, amesema ghafla akaja dada ambaye alikuwa kama anaongea na simu akiwa  ametundika koti la kidaktari kwenye bega na  kumwendea moja kwa moja alipokuwa na kuanza kumwongelesha kwa kumuuliza mtoto amejisaidia na kumjibu ndio.

"Baada ya kumaliza kumsafisha mtoto nami nikawa nasikia haja ndogo, hivyo nikamuomba anisaidie kumshika mtoto na pochi yangu pia nikamwachia nikiamini ni mtu mwema kwani hata choo yeye ndio kanionyesha kilipo jambo linalodhihirisha kuwa ni mwenyeji katika eneo hilo,"amesema Sharifa.

Hata hivyo, amesema baada ya kurejea eneo hilo dada huyo hakumkuta wala kumuona mtoto isipokuwa alimuachia tu pochi na baada ya kuwauliza watu waliokuwepo hapo, wakamjibu naye alikuwa anawaambia kuwa anamtafuta yeye.

"Ndio hivyo tena baada ya kuona hivyo nikatoa taarifa kwa wafanyakazi wa pale ambapo  tukaanza kutafutatafuta pale bila ya mafanikio," amesema Sharifa.

Akieleza namna anavyoishi kwa sasa, Sharifa amesema maziwa yamekuwa yakimtoka tu na hana namna ya kuyazua jambo ambalo ukiacha kumuumiza kimwili pia inamuathiri kisaikolojia kwa kuwa hajui mwanae kama bado yupo mzima au la.

Kwa upande wake baba wa mtoto, Taliq Abdallah, amesema taarifa za kuibwa kwa mtoto wake alizipata akiwa njiani kurejea nyumbani.

Abdallah amesema hiyo siku anakumbuka alimpeleka mke wake hospitali majira ya saa moja asubuhi na kumuacha hapo kisha akaelekea kwenye shughuli zake maeneo ya Mbezi.

Hata hivyo, wakati akiwa anarejea nyumbani akiwa maeneo ya Kigogo kwenye muda wa saa sita mchana ndio akapigiwa simu na mkewe na kumtaarifu kuwa ameibiwa mtoto.

"Nilipomuhoji imekuwaje, akanielezea mkasa mzima ulivyokuwa hadi mtoto kuibiwa jambo ambalo lilinishtua kwa kweli na kujiuliza maswali mengi," amesema Abdallah.

Kutokana na hilo, baba huyo ameviangukia vyombo vya dola na Serikali kwa ujumla kuongeza bidii katika kumtafuta mtoto wake.

"Naomba mamlaka zitumie njia zake zote niweze kumpata mtoto wangu kwa kuwa mbali ya mtoto kuwa mdogo, sijui huko alipo anakula nini na anaishije, maumivu tunayoyapitia kama wazazi Mungu mwenyewe ndio anajua.

"Mbaya zaidi ni kwamba kinga aliyokuwa amepekwa kuipata kwa ajili ya kumkinga na maradhi mbalimbali hiyo siku, ni wazi kwamba usalama wa afya yake pia utakuwa mdogo," amesema Abdallah.

Pia, ametumia nafasi hiyo  kushauri kuwekwa kwa sheria kali katika hospitali watu wanapokwenda na kutoka kwa ajili ya huduma ya mama na mtoto ikiwemo kuuliza kadi ya mama na mtoto wakati wa kuingia na kutoka katika taasisi hizo ili kuweza kuzuia vitendo hivyo.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Mohamed Mang'una, alipotafutwa kuhusiana na tukio hilo, alikiri limetokea japo amesema hayupo katika nafasi nzuri ya kulizungumzia kwa sasa kwa kuwa  lipo katika mamlaka za uchunguzi.