Waliofanyakazi na Baba wa Taifa wapewa tuzo

Muktasari:

  •  Ikiwa zimebaki siku chache Muasisi wa Taifa la Tanzania Hayati Mwalimu Julius Nyerere kama angekuwa hai angetimiza miaka100 ya kuzaliwa kwake, waliokuwa wakifanya naye kazi kwa ukaribu wametunukiwa tuzo za kutambua mchango wao walioutoa kwa taifa na kwa Mwalimu katika harakati za kupigania uhuru.


Dar es Salaam. Ikiwa zimebaki siku chache Muasisi wa Taifa la Tanzania Hayati Mwalimu Julius Nyerere kama angekuwa hai angetimiza miaka100 ya kuzaliwa kwake, waliokuwa wakifanya naye kazi kwa ukaribu wametunukiwa tuzo ya kutambua mchango wao walioutoa kwa taifa na kwa Mwalimu katika harakati za kupigania uhuru.

Miongoni wa waliopewa tuzo hizo ni mke wa Mwalimu Mama Maria Nyerere, Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku.

Wengine ni aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamini Mkapa, Waziri Mkuu wa pili wa Serikali ya Tanganyika Rashid Kawawa, Bibi Titi Mohamed pamoja na Mwenyekiti wa Umoja wa Jumuiya za Wanawake katika nchi huru za Afrika (PAWO) Leah Lupembe.

Tuzo hizo zimetolewa jijini Dar es Salaam jana na Taasisi ya Repatriation Root Tour wakati wa hafla ya kumuenzi Mwalimu Nyerere kuelekea kutimiza miaka 100 ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwake ambapo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Suleiman Jafo alikuwa mgeni rasmi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Jafo amesema anawapongeza wale wote waliotoa wazo la kutoa tuzo ambazo zinatambua mchango wa watu waliojitoa kushirikiana na Mwalimu Nyerere kuhakikisha uhuru wa taifa hili unapatikana.

Amesema taifa la Tanzania lina historia ndefu na wapo wazee wengi wanajua mambo mazito yanayoashiria kuwa nchi imetoka mbali hivyo hawana budi kuwapongezwa na kupatiwa tuzo hizo kama kuheshimu mchango wao katika maendeleo ya nchi.

Naye Mmoja wa waanzilishi wa taasisi hiyo ya Repatriation Root Tour, Debora Nyakisinda amesema wakati taifa litakaposheherekea miaka 100 ya Mwalimu Nyerere, wao waliona ni vema kuwakumbuka watu ambao walimsaidia Mwalimu kufanya mambo makubwa kwa kuwapatia tuzo.

"Tunaposheherekea uthamani wa Mwalimu Nyerere tuwakumbuke ambao walimsaidia kufanya mambo makubwa ambayo yamekuwa historia katika taifa letu, tunaomba pia Serikali ikiwapendeza iwakumbuke watu hawa kwani ni muhimu katika taifa letu," amesema

Kwa upande wake Mwakilishi wa Asasi za Mameya wa Marekani Weusi, Vanessa William amesema wanaelewa kuwa Mwalimu Nyerere alifanikisha kuleta uhuru bila kumwaga damu hivyo ni heshima kwao kuendelea kumkumbuka kwa mambo mazuri aliyoyafanya.


Mwalimu Nyerere alizaliwa Aprili 13, mwaka 1922, alifariki dunia Oktoba 14, 1999 huko London nchini Uingereza alikokwenda kwa matibabu, Mwalimu  alikuwa Rais wa Kwanza wa Tanzania kati ya Oktoba 29 mwaka 1964 hadi Novemba 5 mwaka 1985.