Waliolipia Sh27,000 Manyara kuunganishiwa umeme

Kaimu Meneja wa Tanesco Mkoa wa Manyara, Hamisi Rahisi

Muktasari:

  • Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) mkoani Manyara limesema litawaunganishia huduma wateja waliolipia Sh27,000 mwaka 2021 kwa utaratibu uliowekwa awali kabla ya bei kubadilishwa hivi karibuni.


Babati. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) mkoani Manyara limesema litawaunganishia huduma wateja waliolipia Sh27,000 mwaka 2021 kwa utaratibu uliowekwa awali kabla ya bei kubadilishwa hivi karibuni.

Akizungumza mjini Babati, Kaimu Meneja wa Tanesco Mkoa wa Manyara, Hamisi Rahisi amesema maeneo yatakayounganishwa umeme kwa bei hiyo ni Kata nane, Vijiji 13 na vitongoji 54 na kwamba gharama hizo zimezingatia mipaka ya miji na vijiji iliyoainishwa na Tamisemi.

"Ni haki ya mteja kupata taarifa sahihi ya ufafanuzi wa bei ya kuunganishiwa umeme , Tanesco  inawahamasisha kuendelea kuomba kutumia huduma ya umeme," amesema Rahisi.

Ametaja baadhi ya maeneo yaliyoainishwa na Tamisemi kwa wilaya ya Babati yatakayolipia kuunganisha umeme kwa bei hiyo ni kata ya Bagara yenye kijiji kimoja cha Nakwa, kitongoji cha Sumbi, Mageni, Bagara, Kayto na Simbaki, kata ya Mutuka yenye vijiji viwili vya Mutuka kitongoji cha Sendo A, Sendo B, Mutuka, Sora na kijiji cha Chemchem kitongoji cha Mororoi na Sora.

Ametaja pia kata ya Bonga kijiji cha Haraa kitongoji cha Urusi, Haraa, Busia na Kigongoni pamoja na  kijiji cha Himiti kitongoni cha Samure, Ayanoma, Mirambi, Ambaraku na Haraa, kata ya Maisaka kijiji cha Kiongozi kitongoji cha Kiongozi, Migungani na Misuna na kijiji cha Malangi kitongoji cha Malangi, Sinai, Sawe na Dudumera.

Rahisi amebainisha kuwa kuanzia sasa mteja wa njia moja ndani ya mita 30 kutoka kwenye miundombinu ya umeme katika maeneo ya mjini atalipia kuanzia Sh320,960 badala ya sh27,000.

Kwa upande wake meneja wa Tanesco wilaya ya Hanang’ Nadhir Yusuf amesema sehemu iliyokuwa na mabadiliko ya bei mpya ni Kateshi mjini ambapo maeneo mengine yote yatalipa Sh27,000.