Waliomshambulia, kumjeruhi polisi watupwa jela miaka mitatu

Muktasari:

Mahakama ya Wilaya ya Arusha imewahukumu kifungo cha miaka miaka jela, wakazi watatu wa jijini Arusha, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumshambulia askari wa Jeshi la Polisi aliyekuwa doria katika eneo la Daraja Mbili.

Arusha. Mahakama ya Wilaya ya Arusha imewahukumu kifungo cha miaka mitatu jela wakazi watatu wa jijini Arusha kwa kosa la  kumshambulia na kumdhuru mwili Mkaguzi wa Polisi, Festo Bilali alipokuwa doria akitekeleza majukumu yake.

Pia mahakama hiyo imeamuru washtakiwa hao kumlipa fidia ya Sh100,000 kila mmoja askari huyo kwa maumivu aliyoyapata walipomshambulia.

Hukumu hiyo imesomwa leo Jumatano Aprili 24, 2024 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Jenifer Edward.

Waliohukumiwa adhabu hiyo ni Simon Lucas, Ahmed Shabani na Mackdonald Mollel maarufu Vandame.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 24/2023, watuhumiwa walikuwa wakikabiliwa na kosa moja la kudhuru mwili kinyume na kifungu cha 241 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu huyo ameeeleza kuwa upande wa Jamhuri katika kesi hiyo uliokuwa ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Tony Kilomo uliweza kuthibitisha kosa hilo pasipo shaka.

Amesema baada ya mahakama kupitia ushahidi wa pande zote mbili, umejiridhisha kuwa watuhumiwa walihusika na tukio hilo na kupitia ushahidi wa mwathirika wa tukio hilo, umethibitisha kweli alishambuliwa.

Hakimu huyo amesema ushahidi huo uliungwa mkono na daktari aliyemtibu baada ya kushambuliwa pamoja na shahidi wa tatu (askari jamii) na shahidi wa nne ambaye naye ni askari polisi, ambao siku ya tukio ndio walimsaidia mwenzao na kumkamata mtuhumiwa wa kwanza (Simon).

“Upande wa Jamhuri umeweza kuthibitisha pasipo na shaka kosa lililokuwa linawakabili watuhumiwa wote watatu na waliweza kuwatambua kwenye gwaride la utambuzi na hapa mahakamani pia na mashahidi wa tatu na nne walikuwa wanawajua washitakiwa hata kabla ya tukio,”ameongeza Hakimu Edward.

Amesema utetezi wa washitakiwa haujatosheleza kuweza kuthibitisha kuwa hawakutenda kosa, pia ukiacha mbali ushahidi wa kusema hawakufanya kosa hilo,wote walikiri kuwepo eneo la tukio siku hiyo.

“Baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili, mahakama imewakuta na hatia na inawahukumu kifungo cha miaka mitatu jela na kulipa fidia ya Sh100,000 kila mmoja kwa mwathirika wa tukio hili,” amesema Hakimu huyo.

Awali, Wakili wa Kilomo ameieleza mahakama kuwa siku ya tukio Oktoba 22, 2022, Saa 6;45 usiku katika  baa ya Blue Pub eneo la Daraja Mbili, askari huyo (mwathirika)  akiwa lindo na wenzake kwenye gari, waliona fujo zinaendelea katika baa hiyo.

Inspekta Bilali alishuka kwenye gari kwa ajili ya kwenda kuangalia, lakini alipofika eneo hilo, mtuhumiwa wa kwanza alianza kumshambulia akishirikiana na wenzake, kwa kumpiga ngumi usoni na maeneo mengine ya mwili wake na kumsababishia majeraha na maumivu.

Alidai baada ya wenzake kuona hali ile, alishuka shahidi wa nne na shahidi wa tatu aliyekuwa karibu na eneo hilo wakaenda kumsaidia mwenzao.

Mbali na kumsaidia mwenzao, pia walimkamata mtuhumiwa wa kwanza katika eneo hilo na wenzake wawili walikimbia na kukamatwa baadaye kwa nyakati na maeneo tofauti.

“Mshtakiwa wa kwanza alianza kumshambulia askari aliyefika hapo kujua nini kinaendelea baada ya kuona kundi la watu likipiga kelele kuwa kuna vurugu katika baa hiyo, mshtakiwa wa pili na tatu nao waliungana naye kumshambulia, kabla ya askari wenzake kwenda kuamua,” ameeleza mahakamani hapo.

Katika utetezi wao, washtakiwa hao walikana kumdhuru askari huyo ila walikiri kufika eneo la tukio.