Walioondolewa kazini kwa vyeti feki kulipwa michango yao

Rais Samia Suluhu Hassan

Muktasari:

  • Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia kuwa watumishi wote walioondolewa kazini kwa kughushi vyeti warejeshewe michango yao waliyochangia kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia kuwa watumishi wote walioondolewa kazini kwa kughushi vyeti warejeshewe michango yao waliyochangia kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Watumishi hao ni wale walioondolewa katika utumishi wa umma katika shughuli maalum la uhakiki wa vyeti lililoendeshwa na Serikali kwa kushirikiana na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) katika kipindi cha kuanzia Oktoba 2016 hadi Aprili mwaka 2017.

Kufuatia uhakiki huo, watumishi wasiopungua 14,516 walibainika kuwa na vyeti vya kughushi na waliondolewa katika utumishi wa umma.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Oktoba 26, 2022 na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako wakati akizungumzia kuhusu uamuzi huo.

“Kufuatilia maelekezo hayo, mifuko ya Hifadhi ya Jamii PSSSF na NSSF itarejesha michango ya wafanyakazi iliyowasilishwa kwenye mifuko hiyo bila kuhusisha michango ya mwajiri,”amesema.

Amesema marejesho ya michango hiyo itaanza kufanyika kuanzia Novemba Mosi mwaka 2022, ambapo mtumishi husika atatakiwa kwenda kwa aliyekuwa mwajiri wake akiwa na picha mbili za passport size.

Vingine anavyotakiwa kwenda navyo ni nakala ya taarifa za benki (Bank Statement) ya akaunti iliyo hai na nakala ya kitambulisho cha Taifa au mpiga kura au leseni ya udereva.

Amesema pia mtumishi atatakiwa kujaza hati ya ridhaa kwa aliyekuwa mwajiri wake.