Wamachinga 150 wakubali kuondoka barabarani

Wafanyabiashara wadogowadogo (machinga) kata ya Mishine wakiwa kwenye kikao cha pamoja cha makubaliono ya kuondoka eneo ambalo ni hataraishi na kuelekea eneo ambalo wamepangiwa kufanyia biashara zao. Picha na Daniel Makaka
Muktasari:
- Wamachinga zaidi ya 150 wa kata ya Misheni wilayani Sengerema mkoani wa Mwanza wamekubali kuondoka kandokando mwa barabara kuepuka ajali .
Sengerema. Wamachinga zaidi ya 150 wa kata ya Misheni wilayani Sengerema mkoani wa Mwanza wamekubali kuondoka kandokando mwa barabara kuepuka ajali .
Makubaliano hayo yamefanyika kwenye kikao cha pamoja na viongozi wa kata hiyo kikiongozwa na Mwenyekiti wa maendeleo ya kata hiyo Francins Mbugai ambaye ni Diwani wa kata hiyo.
Mbugai amesema kuwa asilimia 75 ya masoko ya jioni yaliyoko kandokando mwa barabara yamesabisha ajali nyingi na watu kupoteza maisha huku wengine wamejeruhiwa.
"Tumekubaliana kuondoka barabarani tumewapatia eneo jingine ambalo liko sahihi watafanya biashara zao bila Shaka yoyote watafanya hadi usiku tutawawekea taa" amesema Mbugai.
Ofisa Mtendaji kata ya misheni Yusuph Mayala amesema kikao cha Wamachinga hao na uongozi wa kata hiyo wamekubalina kuondoka eneo lisilo rasmi baada ya kupatiwa eneo jingine kwa ajili ya kufanyia biashara zao.
“Watu wawili wamepoteza maisha kwa kugongwa na gari katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita huku 30 wakijeruhiwa wakati wanakwenda kununua bidhaa mbalimbali kwenye katika soko la jioni kwenye kata ya Mishine wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza " amesema Ofisa Mtendaji kata ya misheni Yusuph Mayala.
Mmoja wa wamachinga kata ya misheni Anastazia Amos, amesema wamekubali kuhama eneo walilokuwepo kutokana na eneo hilo kutokuwa salama na kuwashukuru viongozi wa kata hiyo kwa kuwapatia eneo jingine ambalo ni salama.
Mwenyekiti wamachinga Kata ya misheni, James Sumuni amesema wamekubaliana kuondoka barabani na kwenda eneo walilotengewa ili kufanya biashara zao.
" Tunashukuru viongozi wa kata ya misheni kwa kutushirikisha katika jambo hili tumekubalina kwa pamoja kuelekea kwenye eneo walilotutengea " amesema Sumuni.