Wamachinga warejea maeneo waliyofukuzwa

Muktasari:

  • Ikiwa imepita miezi minane tangu Serikali iwaamuru wafanyabiashara ndogondogo (wamachinga) wahame katika maeneo yasiyo rasmi, wameanza kurejea huku wakibadili mbinu za ufanyaji biashara.

Dar es Salaam. Ikiwa imepita miezi minane tangu Serikali iwaamuru wafanyabiashara ndogondogo (wamachinga) wahame katika maeneo yasiyo rasmi, wameanza kurejea huku wakibadili mbinu za ufanyaji biashara.

Septemba 2021, Rais Samia Suluhu Hassan aliwaagiza wakuu wa mikoa nchini kuwapanga wamachinga katika maeneo stahiki bila kusababisha vurugu.

Licha ya ugumu kuwaondoa wafanyabiashara katika maeneo hayo, hatimaye baadhi ya wakuu wa mikoa wakiwatumia mgambo wa halmashauri za wilaya, manjispaa na majiji walifanikiwa kuwaondoa.


Warejea

Baada ya kuondolewa kwa wafanyabiashara hao, baadhi yao walibuni mtindo mpya wa kurejea kwenye maeneo yao nyakati za jioni, wakati ambao mgambo hawapo, huku wengine wakirejea polepole maeneo ya katikati ya majiji.

Mwananchi limetembelea maeneo walikorejea wafanyabiashara na kuzungumza nao.

Ramadhani Kassim, anayefanya biashara eneo la Mnazi Mmoja alisema, baada ya Serikali kuwahamishia kwenye soko la Kisutu na Machinga Complex, aliamua kurudi kutokana na biashara anayoifanya.

“Ni kweli Serikali ilituondoa hapa kituoni, lakini mimi biashara yangu nategemea abiria na wapitanjia, ninachofanya bidhaa zangu nimezificha sehemu, ninapomuona mtu anaulizia naenda kumbchukulia,” alisema Kassim.

Naye Janet Ishengoma alisema anafanya biashara ya kuuza chakula kwa kuibaiba, kwani mgambo wamekuwa wakiwakamata na kuwanyang’anya na kuvipeleka vifaa wanavyotumia ofisi za mitaa.

Mkoani Mbeya, licha ya Serikali kujenga soko la kisasa la wafanyabishara hao katika eneo la uwanja wa ndege wa zamani, bado wamekuwa wakirejea katika maeneo waliyoondolewa.

Salome Jamse, mfanyabiashara wa bidhaa za urembo na mbogamboga alisema Serikali kabla ya kujenga soko katika eneo hilo ingefanya tathimini ya umbali wa upatikanaji wa huduma za kijamii.

“Ukiangalia Soko la awali la Sido na Mwanjelwa yapo katikati na jamii inapata huduma kwa urahisi, sasa huko uwanja wa ndege ni mbali na hivyo tunaona ni vyema kutandika bidhaa chini ili wateja wetu wasipate tabu kutembea umbali mrefu,” alisema.

Hata hivyo, katika jiji la Arusha hali sio tofauti na majiji mengine, wafanyabiashara wa matunda na mbogamboga wameanza kurejea barabarani katika Jiji hilo.

Wafanyabiashara hao wamekuwa wakijitokeza jioni maeneo kadhaa, ikiwepo kituo Kikuu cha mabasi, nje ya masoko ya Kilombero, Soko Kuu na katika maeneo mengine katikati ya mji.

Mfanyabiashara Hyacinta Noel alisema wameamua kuuza mbogamboga nje ya soko ili kufuata wateja kwa kuwa biashara ni ngumu.


Machinga Dar

Akizungumzia madai ya wafanyabiashara kurudi kwenye maeneo waliyofukuzwa, Mwenyekiti wa Chama cha Wamachinga Mkoa wa Dar es Salaam, Namoto Yusuf alisema wameshawaonya wanaorudi, kwani wanapoteza fursa ya utetezi na kupata mikopo ya biashara.

Alisema kwa sasa wameingia makubaliano na Benki ya Maendeleo na wameshatoa mikopo kwa jumla ya wamachinga 1,000 yenye thamani zaidi ya Sh1.58 bilioni.

Jijini Mwanza nako wameanza na kurejea kwenye maeneo waliyokatazwa kufanya biashara.

Kabla ya kuanza operesheni ya kuwapanga, wamachinga katika jiji hilo walikuwa wakipanga bidhaa zao kwenye barabara, mitaro, mbele ya maduka na taasisi za umma, jambo lililosababisha usumbufu kwa wapitanjia na watumiaji wengine.

Masoko yalitengwa kwa ajili ya wamachinga kufanya biashara zao, ikiwemo Soko la Mchafukoge lililoko kata ya Igogo, soko la Buhongwa (Dampo), Bango la Zein Kata ya Kisesa na soko la Mboga na Matunda lililoko Kilimahewa wilayani Ilemela mkoani humo.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Machinga Tanzania (Shiuma) Mkoa wa Mwanza, Mohammed Dauda alisema wafanyabiashara hao wanarejea maeneo waliyoondolewa kutokana na masoko yaliyojengwa kukosa miundombinu na wateja wa kutosha wa bidhaa zao.

Pia alilalamikia maeneo yalipo masoko hayo kukosa mwingiliano wa watu, masoko hayo kufungwa inapofika Saa 12 jioni, huku akidai wamachinga wanafanya biashara hadi nyakati za usiku.

Mmachinga katika mtaa wa Rwagasore, Mwita Chacha alisema alipohamishiwa katika soko la Mchafukoge alikuwa na mtaji wa Sh1.2 milioni na hadi Juni 23, 2022 alisaliwa na mtaji usiozidi Sh50,000.


Kauli za viongozi

Mwenyekiti wa wafanyabiashara katika Jiji la Arusha, Adolf Masawe alisema kuanza kurudi wafanyabiashara ni kero kwa wafanyabiashara wa maduka na watumiaji wa barabara.

Msemaji wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, Stephen Chamle alisema wamekuwa wakiathiriwa na wafanyabiashara ndogondogo (wamachinga) kwa kuchanganywa eneo moja na pia hawalipi kodi.

Alibainisha kuwa Serikali iliposema itajenga maeneo maalumu ya wamachinga, kauli ile iliwapa faraja, lakini bado hawajaona jitihada zozote zaidi ya kuwahamisha na kuwachanganya.

“Unamchanganyaje mmachinga na mfanyabiashara mkubwa sehemu moja, wamekuwa hawalipi kodi, mbaya zaidi wanafanya biashara kwenye maeneo ya maegesho ya magari mbele ya biashara zetu,” alisema Chamle.


Mbinu wanazotumia

Ili kukwepa kukamatwa na askari mgambo wafanyabiashara hao wamekuwa wakipanga vitu juu ya mifuko iliyofungwa kamba, ili wanapotaka kukamatwa iwe rahisi kukimbia na bidhaa zao.

Mbinu nyingine ni kuhifadhi bidhaa zao kwenye ofisi za watu, na kubaki na mfano wa bidhaa anayouza, atazunguka nayo na pale atakapopata mteja, huuza bidhaa hiyo au kwenda kumchukulia nyingine.

RC Gabriel

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel alisema utaratibu wa kuwapanga na kuwaondoa machinga katika maeneo hatarishi ni endelevu.

Imeandikwa na Fortune Francis (Dar), Hawa Mathias (Mbeya), Mussa Juma (Arusha) na Mgongo Kaitira (Mwanza)