Wamiliki wa mabasi wakusudia kusimamisha huduma ya kusafirisha abiria

Muktasari:

  • Wamiliki wa mabasi wanakusudia kusimamisha huduma zao wakitaka maelezo ya kutosha kuhusu matumizi ya mashine za kukatisha tiketi kwa mtandao (POS) wakisema mfumo huo unawaumiza kibiashara.

Dar es Salaam. Wamiliki wa mabasi wameeleza kusudio lao la kusimamisha huduma ya kusafirisha abiria endapo suala la kutumia mashine za kukatia tike kwa njia ya mtandao (POS) halitapatiwa ufumbuzi.

Mashine za POS zinamtaka mmiliki wa fedha kuweka kiasi cha fedha  katika laini ya simu  au wakala wa huduma za  fedha kwa makadirio ya abiria wa basi husika. Mfano kama basi linabeba abiria 50 kwa nauli ya Sh30,000, mmiliki analazimika kuweka Sh1.5 milioni katika laini ya mashine hiyo.

Hata hivyo, kwa nyakati tofauti baadhi wa wamiliki wamekuwa wakiulalamikia mfumo wakisema siyo rafiki kwa matumizi ya mabasi hayo wakidai una mapungufu makubwa yanayosababisha wao kupata hasara.

Kutokana na hali hiyo, leo Jumamosi Machi 6, 2021 Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), kimeitisha kikao cha dharura kwa ajili ya kujadili mfumo huo ambapo asimilia kubwa wa wajumbe wa mkutano huo waliazimia kuegesha mabasi yao endapo suala hilo halitashughulikiwa.

Wengine wameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (Latra), kuachana na mfumo huo badala watoe muongozo kwa wamiliki kutumia mashine za kieletroniki za EFD zinazotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Ingawa hakuwasema muda wa utekelezaji wa mchakato huo wa kuegesha mabasi yao, lakini walitaka Latra kulishughulikia suala hilo, wakisema tangu kuanza kutumika wamekuwa wakipata hasara hali inayosababisha kutojiendesha kwa ufanisi.

“Hili suala ni janga inabidi tupate mashine nyingine kama wanazotumia wafanyabishara. Endapo mfumo huu utaendelea  nitawalipa wafanyakazi wangu madai yao kisha mabasi yangu nitayaegesha maana sitoweza,” amesema Max Komba mwakilishi wa mabasi ya Tavavili.

Mwaka 2017 Taboa mkutano mkuu maalumu wa Taboa uliazimia kugoma kutofanyika kwa shughuli za usafirishaji , wakipinga sheria inayolenga kupitishwa ambayo walidai haikuwashirikisha wadau na haitenganishi makosa ya dereva na mmiliki, hali inayosababisha kosa lililofanywa na dereva kusababisha mmiliki kufungwa jela.