Wamiliki wa shule binafsi walalamikia zuio shule za bweni

Muktasari:

Tamongsco yaeleza masikito yao ya kutoshirikishwa katika utolewa wa waraka unaotolewa na ofisi ya kamishna wa elimu, yasema itamwandikia barua Rais Samia kumweleza hali hiyo.

Dar es Salaam. Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi nchini (Tamongsco), kimedai kutoshirikishwa katika waraka unaotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ukiwemo wa kusitishwa kwa huduma ya bweni kwa madarasa ya kwanza hadi la nne.

Mwenyekiti wa Tamongsco, Alfred Luvanda ameeleza hayo leo Alhamisi Machi 23, 2023 wakati akizungumza na Mwananchi, nje ya kikao cha wanachama wa umoja huo waliokuwa katika kikao cha dharura chenye lengo la kujadili waraka huo.

“Kuna waraka kama mitatu hivi hatukushirikishwa ikiwemo mihula, ratiba za masomo na waraka wa ada elekezi, hatukushirikishwa na mamlaka husika,” amesema.

Kutokana na hilo, Luvanda amesema Tamongsco inakusudia kumwandikia barua Rais Samia Suluhu Hassan, kumueleza hatua ya kutoshirikishwa kwao katika waraka wa kusitishwa kwa huduma ya bweni kwa madarasa ya kwanza hadi la nne, uliobua sintofahamu kwa wamiliki wa shule binafsi.

Luvanda amesema watamweleza Rais Samia athari zitakazojitokeza baada ya waraka huo, wakisema baadhi ya wamiliki wametumia gharama na fedha nyingi katika ujenzi wa mabweni na walifuata taratibu zote ikiwemo vibali katika kuyaanzisha.

“Leo mtu anaposema funga bweni, hivi unajua kuna fedha imewekezwa? Tutapata hasara ya jumla. Lakini kuna walezi wanaotoa huduma katika mabweni, sasa kwa tangazo la Serikali maana yake hawana kazi,” amesema.

Mbali na hilo, Luvanda alisema Tamongsco itaandaa waraka wake unaohusu changamoto wanazokabiliana nazo na kutishia uhai wa utoaji wa huduma hiyo. Pia namna Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inavyotoa waraka mfululizo inayodaiwa kuwapa wakati mgumu.

Machi 6 mwaka huu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imezitaka shule zote zinazotoa huduma ya bweni kwa madarasa ya kwanza hadi la nne kusitisha huduma hiyo ifikapo mwisho wa muhula wa kwanza mwaka 2023.

Waraka huo ulitolewa na Kamishna wa Elimu wa wizara hiyo, Dk Lyabwene Mtahabwa kwa wadau wa elimu nchini, akisema utekelezaji wa waraka huo unatakiwa kuanza Machi Mosi mwaka huu.

Dk Mtahabwa alisema hairuhusiwi kutoa huduma ya bweni kwa wanafunzi wa elimu ya awali na darasa la kwanza isipokuwa kwa kibali maalum kitakachotolewa na Kamishna wa Elimu baada ya kupokea maombi kutoka mdau husika.

Katika kikao hicho cha leo wanachama wa Tamongsco wamesema hawapingi hatua ya Serikali kutoa waraka, lakini kinachotakiwa utaratibu ufuatwe katika mchakato huo ikiwemo ushirikishwaji wa wadau.

“Tunamuomba Mama (Rais Samia), aingilie kati, maana wizarani kuna ombwe, hali ikiendelea itasababisha matatizo. Kwa mamlaka aliokuwa nayo atoe tamko ya haya matishio, yanaziweka shule binafsi katika wakati mgumu.

“Tunatamani Rais Samia ajue na atusaidie kwa sababu kufungia mabweni ni ukatili dhidi ya sekta binafsi. Rais Samia akisikia angalie namna kushawishi Bunge na mamlaka za kisheria kuondoa waraka zote kandamizi,” amesema Luvanda.

Luvanda amesema lazima suala hilo, lipatiwa ufumbuzi ili wizara husika ikizungumza jambo lolote basi liwe linatoka katika kamati ya ushauri. Amesema wana imani na Rais Samia atalipatia ufumbuzi, kwa sababu ameshafanya hivyo, katika maeneo mengine.

“Tutakusanya sahihi za wajumbe wote waliohudhuria mkutano huu, kisha tutamwandikia barua moja kwa moja Rais Samia. Hatutaki kuandamana, wala kugombana na Rais Samia,” alisema Luvanda.

Mwananchi lilimtafuta Dk Mtahabwa, kuhusu malalamiko ya Tamongsco ambapo amesema, hakuwa na taarifa za kikao hicho.

“Wameongea nini au wameazimia nini, hadi yafike mezani kwangu niweze kuyajibu,” amesema Dk Mtahabwa.

Kwa mujibu wa Luvanda, kuna matamko zaidi ya sita yameshatolewa hadi hivi sasa na taasisi zikitoa mrejesho kwa Serikali, ofisi ya kamishna wa elimu inayaondoa. Hata hivyo, Tamongsco imeazimia kukabiliana na changamoto hiyo hivi sasa.

Awali wakichangia katika kikao hicho, baadhi ya wamiliki na mameneja wa shule uwepo wa mabweni kwa madarasa hayo, unasaidia sio tu kwa watoto wenye uwezo bali hata wale wanaoishi katika mazingira magumu.

“Kuna watoto wanaishi katika mazingira magumu mabweni haya yanawasaidia, sasa yakiondolewa sijui itakuaje kwa sababu baadhi yao watalazimika kutembe umbali mrefu hasa maeneo ya vijijini,” amesema Boniphase Mariki, mmiliki wa shule kutoka Morogoro.

Lawena Nsonda kutoka Mbeya, amesema mabweni yanawasaidia watoto kuepukana na vitendo hatarishi na viovu, akisema maazimio yatakayofikiwa katika kikao hicho, atayaunga mkono.

Mmiliki mwingine, mchungaji Glonous Shoo kutoka mkoani Kilimanjaro amesema suala hilo linahitaji maridhiano, ili kuondoa hali ya kundi moja kuumia na jingine kunufaika.