Prime
Wamiliki watoa hoja 30 wakitaka upya wa mchakato wa 'Sinza mpya'
Muktasari:
- Serikali imetangaza mpango wa miaka 20 wa kuliendeleza eneo lote la Sinza, mchakato ulioanza mwaka 2026-2046, ukilenga kufanya eneo hilo kuwa jumuishi la makazi na biashara na miundombinu mingine
Dar es Salaam. Wamiliki wa ardhi katika eneo la Sinza wamewasilisha hoja 30 kwa Wizara ya Ardhi, zikijumuisha pingamizi, maombi ya ufafanuzi na mapendekezo kuhusu rasimu ya mpango wa uendelezaji upya wa eneo hilo kwa mwaka 2026 hadi 2046, wakitaka mchakato huo uanze upya.
Katika hoja hizo walizozitoa jana Jumapili Juni 14, 2026, wamiliki hao wamependekeza mchakato kuanza upya, wakitaka kuwepo kwa uwazi na kuimarishwa kwa ushirikishwaji wao katika hatua zote za uamuzi.
Mbali na mapendekezo hayo, wametaka ufafanuzi wa hoja 30 ikiwamo ya uunganishwaji wa viwanja vyao ambayo Serikali ilibainisha kuna viwanja vitaunganishwa hadi vinane kuwa kimoja.
Pia, wametaka ufafanuzi wa kupoteza umiliki wa moja kwa moja wa ardhi, kuhamishwa kwa muda kwenye makazi yao ya sasa wakati wa ujenzi na haki ya kurejea, pamoja na uthamini na fidia kwa wale wanaotumia maeneo yao kama kitega uchumi kwa kupoteza mapato mradi ukianza.
Katika mkutano huo, wamiliki hao wamekuja na randama yenye hoja hizo, wakienda mbali zaidi kwamba endapo itaibuka migogoro ya umiliki wa pamoja na kutatokea kushindwa kwa mradi au wawekezaji kujiondoa, watalindwaje kisheria.
Wamedai mchakato huo hivi sasa unaendelea lakini hakuna elimu ya kutosha kwa umma kuhusu mpango huo huku wakihoji kwa nini mahudhurio ya wamiliki katika vikao yanachukuliwa kama ridhaa, wakionya pia kuwepo kwa ukosefu wa uwazi hususani wa wawekezaji.
Mwenyekiti wa kamati ya wamiliki wa ardhi Sinza, Lumuli Mwaipopo amesema wameamua kuja na randama ya hoja hizo ili kutaka uwazi na ushirikishwaji katika kila hatua huku wakidai licha ya rasimu ya ujenzi wa Sinza mpya kuonesha wamiliki walipewa taarifa Agosti 2024, lakini wengi wameufahamu mchakato huo Aprili, mwaka huu.
"Tulimuuliza diwani juu ya taarifa hizo kwa wamiliki, akasema alipitisha gari mtaani kutangaza, Sinza ina wamiliki tofauti wapo wanaoishi hapo na wanaoishi nje ya Sinza.
"Kama mlengwa wa mpango huo alikuwa ni mmiliki ungetolewa wito wa maandishi ili kumfikia kila mmiliki kupitia hata wapangaji wake na si kupitisha gari la matangazo," amesema Mwaipopo.
Amesema hawapingi maendeleo, bali wanahitaji uwazi na ushirikishwaji katika mchakato mzima, akibainisha kwamba katika hilo wamepeleka maombi Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuomba mchakato huo uanze upya na wamiliki washirikishwe katika kila hatua.
Waziri wa wizara hiyo, Dk Leonard Akwilapo alipoulizwa na Mwanannchi kuhusu hoja za wamiliki hao kama amezipokea na maombi ya kutaka mchakato uanze upya, alielekeza aulizwe Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Dk Aron Kagurumjuli.
Amesema mpango huo unasimamiwa na Mkurugenzi wa mipango miji Wizara ya Ardhi, Deogratius Kalimenze.
Hata hivyo, alipotafutwa kwa simu hadi saa 11 jioni ya Juni 15, 2026 simu yake imeita bila kupokelewa.
Kwa mujibu wa randama ya wamiliki hao, masuala mengi yaliyomo katika rasimu wanaona hayajagusa moja kwa moja haki za umiliki wa ardhi, masilahi ya kiuchumi ya wananchi na mustakabali wa wakazi wa Sinza kwa jumla.
Miongoni mwa hoja zilizopewa uzito mkubwa ni suala la kuunganishwa kwa viwanja, baadhi ya wamiliki wana hofu kwamba hatua hiyo inaweza kupunguza uhuru wao wa kuamua matumizi ya ardhi na kuwalazimu kuingia katika mifumo ya umiliki wa pamoja bila dhamana za kutosha za kisheria.
Pia, wameonesha wasiwasi kuhusu uwezekano wa kupoteza mapato ya upangishaji wa nyumba wakati wa utekelezaji wa mradi, kutokuwepo kwa uhakika wa kurejea katika eneo baada ya maendeleo, pamoja na hofu ya kuongezeka kwa gharama za maisha na huduma ambazo zinaweza kuwafanya wakazi wa sasa kushindwa kumudu kuendelea kuishi katika eneo hilo.
Nyingine ni uwazi kuhusu wawekezaji watakaohusika, chanzo na uhakika wa ufadhili wa mradi, pamoja na uwepo wa mifumo madhubuti ya kushughulikia migogoro inayoweza kujitokeza wakati na baada ya utekelezaji wa mpango huo.
Pia, wametaka ufafanuzi wa athari kwa mirathi na vizazi vijavyo na mfumo wa kisheria wa kutatua migogoro baada ya mradi.
Mwananchi ilimtafuta Ofisa Mipango Miji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Emily Mwasogye ambaye katika mkutano na wamiliki, ndiye alikuwa akiuelezea kwa kina mradi huo na kutaka kufahamu ulipofikia na namna wanavyoshughulikia changamoto zinazobainishwa na wamiliki, alijibu kwa kifupi sio msemaji.
Hata hivyo, katika mkutano wa Aprili 19, 2026, Emily alibainisha namna mchakato huo utakavyofanyika na kueleza kwamba katika suala la kuunganisha viwanja, kuna maeneo yatalazimika kuunganishwa vinane ili kupata kimoja.
Kuhusu wawekezaji, alisema mchakato bado unaendelea kwa wamiliki watakaoweza kuendeleza wenyewe au mwekezaji wao, wataendeleza kwa kutumia ramani ya Sinza mpya na kutakuwa na wawekezaji ambao watatafutwa na wizara.
Kuhusu maeneo ya kuishi wakati ujenzi unaendelea, hilo pia walieleza litazigatiwa mara mradi utakapoanza huku pia ukitoa mwanya kwa wamiliki watakaopenda kuuza au kukodisha maeneo yao kufanya hivyo.
Hivi karibuni, Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Eleuteri Mangi alieleza kuhusu mpango wa uendelezaji upya wa eneo la Sinza na kubainisha kuwa Waziri Akwilapo alisisitiza ushirikishwaji wa wananchi na wamiliki wa ardhi, akiwataja kama wadau wakuu katika mchakato huo unaoendelea.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Mangi alisema Serikali inaendesha mikutano ya uhamasishaji na ushirikishwaji wa wananchi katika ngazi mbalimbali, kuanzia mitaa hadi ngazi za juu, ili kuhakikisha kila hatua ya mpango huo inafahamika na kukubaliwa na wadau husika.
Aidha, alisisitiza kuwa Serikali inawataka wananchi kuwa makini na taarifa za upotoshaji zinazoweza kusambazwa na watu wasio na nia njema, akibainisha kuwa wakazi wa Sinza na nchi kwa ujumla watafaidika na mpango huo unaolenga kuboresha ustawi wa kijamii na kiuchumi.
Alisema uendelezaji wa eneo la Sinza unalenga kukabiliana na ongezeko la kasi la watu mijini pamoja na mahitaji yanayoongezeka ya shughuli za kiuchumi na huduma za kijamii katika Jiji la Dar es Salaam.
“Eneo hili lina nafasi kubwa ya kuwa kitovu cha makazi ya kisasa, biashara, huduma za kijamii na uwekezaji, kwa kuzingatia Mpango wa uendelezaji upya wa Sinza wa miaka 20 kuanzia 2026 hadi 2046,” alisema Mangi.
Aliongeza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeweka mwelekeo wa mageuzi ya kujenga Tanzania jumuishi, yenye uchumi wa kisasa unaotegemea maarifa, teknolojia, ushindani wa miji na mazingira bora ya kuishi, mambo ambayo yanachangia usalama, utulivu na ukuaji wa uchumi.
Mangi alibainisha pia kuwa dhana ya uendelezaji upya wa maeneo ya mijini si mpya nchini, akitolea mfano wa maeneo ya Dar es Salaam ambayo tayari yamepitia mabadiliko makubwa ya kimatumizi na kiuchumi kupitia mipango ya maendeleo, ikiwamo Posta, Upanga, Kariakoo, Magomeni, Oysterbay, Masaki, Ilala, Buguruni, Kurasini na Temeke.