Wanafunzi 26 pekee wafaulu mtihani wa uwakili

Muktasari:

  • Anguko kwenye mtihani wa uwakili katika Shule Kuu ya Sheria Tanzania (LST) limefikia hatua mbaya na kuwaibua wanasheria na wadau wengine wakitaka utafiti ufanyike kubaini chanzo cha tatizo hilo.

  

Dar es Salaam. Anguko kwenye mtihani wa uwakili katika Shule Kuu ya Sheria Tanzania (LST) limefikia hatua mbaya na kuwaibua wanasheria na wadau wengine wakitaka utafiti ufanyike kubaini chanzo cha tatizo hilo.

Pendekezo hilo na mengine yamekuja kufuatia matokeo mabaya kupindukia katika mtihani uliofanywa mwaka huu na wanafunzi 633.

Katika mtihani huo wanafunzi 26 (sawa na asilimia 4.1) pekee wamefaulu, 342 wametakiwa kurudia baadhi ya masomo (suplimentary) huku wengine 265 (asilimia 41.9) wakifeli na kukatishwa masomo (dicontinued).

Hali hiyo, ingawa si jambo jipya katika shule hiyo, mwaka huu imepindukia ukilinganaisha na miaka mingine ya karibuni.

Katika mwaka wa masomo 2018/2019 kati ya wanafunzi 1,735 waliofanya mtihani 347 (asilimia 20) walifaulu kuendelea, 484 walirudia mitihani na 468 (asilimia 26.9) walifeli.

Kadhalika, mwaka wa masomo 2016/17-2017/18 kati ya wanafunzi 2,662 waliofanya mtihani 445 (sawa na asilimia 16.72) walifaulu, 1,611 (sawa na asilimia 60.53) walirudia na 606 (sawa na asilimia 22.76) walifeli.

Uongozi wa shule hiyo umejibu malalamiko ya wadau ukifafanua changamoto zilizopo, ikiwemo ya maandalizi duni waliyoyapata wanafunzi hao katika vikuu vikuu mbalimbali walivyosomea shahada zao.

Utafiti ufanyike

Akizungumzia hali hiyo, Jaji wa Mahakama Kuu, Gabriel Malata alisema jawabu la changamoto zote zinazoikabili hatua hiyo ya taaluma ya sheria litapatikana iwapo utafanyika utafiti.

“Kabla hatujaenda mbali lazima tujue tatizo na kuliwekea nguvu, bila shaka ufumbuzi utapatikana. Tujue kwanini hali hii inajitokeza? Mtalaa unaweza kuwa sehemu ya tatizo lakini tukifanya utafiti tutabaini na mengine mengi,” alisema.

Kwa kuwa jambo hilo linahusu maisha ya watu, Jaji Malata alisema si vema mwanafunzi anahitimu shahada kisha anakwama miaka kadhaa katika Shule Kuu ya Sheria, sababu anafeli.

“Watu wanakukuruka hawatoki, watu wamemaliza shahada zao, ni nguvu kazi hao, wakiachwa watachangia uchumi, lakini kwanini wanashindwa kutoka, haya yote yafanyiwe stadi kujua tatizo. Swali gumu lina majibu magumu pia,” alifafanua.

Mtazamo wa Jaji Malata unaungwa mkono na Wakili Fulgence Massawe aliyesema kuna haja ya kuundwa tume kuchunguza tatizo lililopo.

Kwa kuwa LST hukutanisha wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali waliofundishwa na mifumo tofauti, alisema tume ya uchunguzi ni muhimu kuundwa.

Mbali na tume, Massawe alitaja changamoto katika ufundishaji wa ngazi hiyo ya sheria kuwa ni mwalimu mmoja kufundisha wanafunzi takriban 800 katika darasa moja.

“Kwa sababu hii, hakuna namna inayomwezesha mwalimu kujua kama ameeleweka au la, lakini hata wanafunzi kuuliza maswali wakati wanafundishwa inakuwa vigumu.

“Tuunde tume ichunguze, tutajua tatizo ni shule ya sheria au walikotoka wanafunzi, lakini tukisema walikotoka, kuna watu wanatoka kwenye vyuo vinavyoaminika lakini wanakwenda pake wanafeli, kuna haja ya kujua lilipo tatizo,” alisema.

Mtalaa watajwa

Mwanataaluma mwingine, Dk Neema Mwita, mhadhiri wa Sheria katika Chuo Kikuu cha St. Augustine (SAUT) Mwanza, alitaja mtalaa wa t sheria kuwa sehemu ya sababu za changamoto ya ufaulu katika masomo hayo.

Katika Shule Kuu ya sheria, alisema mwanafunzi anajifunza kwa vitendo kile alichokisoma kwa nadharia alipokuwa chuo kikuu, hivyo huo unakuwa utaratibu mpya katika masomo yake.

Alishauri mtalaa wa sheria chuo kikuu uweke ulazima wa mafunzo kwa vitendo kwa kila mwanafunzi wa sheria, ili anapofika Shule Kuu ya Sheria asikutane na vitu vipya.

“Katika masomo ya shahada kuwe na fani ya kuandaa nyaraka za kisheria ili mwanafunzi akifika Shule Kuu ya Sheria angalau awe anajua, maana hivi ndivyo vitu anavyokwenda kujibia mtihani,” alisema.

Iwapo kila chuo kitakuwa na utaratibu huo, alisema idadi ya wanaofeli itapungua kwa kuwa tayari watakuwa na msingi mzuri.

Mfumo wa ufundishaji

Mmoja wa wanafunzi wa LST (jina limehifadhiwa), alitaja mfumo wa ufundishaji kuwa tatizo katika matokeo hayo.

Alisema mafunzo katika shule hiyo hutolewa kwa muda mfupi, ikiaminiwa kuwa tayari mwanafunzi alishasoma akiwa chuo kikuu, jambo ambao si kweli.

“Somo moja mnamaliza kwa wiki moja, somo hilo hilo mlipokuwa chuoni mlisoma kwa mwaka mmoja, vitu havifanani, wao wanaamini mlishajifunza lakini uhalisia ni kwamba mnakutana na mambo mapya,” alisema.

Alishauri shule hiyo ipunguze idadi ya wanafunzi wanaosajiliwa na iongeze muda wa masomo ili kuongeza ufaulu.

“Bora LST ichukue wachache na wasome kwa muda mrefu ili ufaulu usibaki kuwa bahati ya wachache,” alisema.

Mwanafunzi mwingine alidai kinachowafelisha wengi ni utaratibu wa shule hiyo ambapo, unachofundishwa sicho utakachoulizwa kwenye mtihani.

Changamoto nyingine , alisema ufundishaji wa chuo kikuu hauhusishi zaidi uchambuzi wa sheria, jambo ambalo linafanyika katika shule ya sheria.

“Chuo Kikuu unaweza kufundishwa na mwalimu asiyepita hata katika Shule Kuu ya Sheria, hajui huku tunakuja kukutana na nini, hatujengewi msingi utakaotuwezesha kuyamudu ya huku,” alisema.

Walivyoandaliwa shida

Akijibu hoja hizo, Makamu Mkuu wa Chuo (Mafunzo ya Sheria kwa Vitendo na Utafiti), Profesa Zakayo Lukumay alisema tatizo kubwa linatokana na namna wanafunzi hao walivyoandaliwa katika vyuo vikuu walivyotoka.

“Waliofundishwa na walimu wazuri wanafaulu, lakini waliofundishwa vibaya ndiyo hao wanaofeli kwa kuwa wanakuja na uelewa mdogo ilhali asili ya mafunzo yetu (shule ya sheria) ni kufanya kwa vitendo,” alisema.

Kinachotokea kwa wanaofeli, alisema maana yake mwanafunzi anashindwa kukitafsiri alichofundishwa kwa nadharia kwenda kwenye vitendo.

Alisema katika shule hiyo kinachofundishwa ni jinsi ya kuifanya kazi ya taaluma husika, mathalan namna ya kumuhoji shahidi na kuandaa nyaraka za kisheria, wakiamini kuwa tayari mwanafunzi huyo alishafundishwa maana ya shahidi.

“Kule chuoni alijifunza kitu kinachoitwa hukumu, kinatakiwa kuwaje, lakini huku shule ya sheria tunamtaka aandike hukumu,” alisema.

Alisema wanaofeli wengi wao, hawajui kufanya vile walivyoelekezwa kwa nadharia.

Kuhusu mitihani, Profesa Lukumay alisema inahusisha kueleza mlolongo wa tukio na mwanafunzi anatakiwa kujibu kwa kushauri kisheria na kuandaa nyaraka zinazohitajika.

Kwa bahati mbaya, alisema wanafunzi wengi wanajibu kwa kueleza utaratibu badala ya kuandaa nyaraka kama ambavyo swali linahitaji na hapo ndipo wanapokosea.