Wanafunzi Mara waruhusiwa kwenda shuleni bila sare

Mkuu wa mkoa wa Mara,  Ally Hapi akizungumza na baadhi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari Dk Nchimbi wilayani Bunda alipotembelea shule hiyo kukagua madarasa matatu yaliyojengwa shuleni hapo kwa fedha za Uviko-19 kwa gharama ya Sh60 milioni.  Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

Serikali mkoani Mara imetoa wa mwezi mmoja kwa wanafunzi wasiokuwa na sare za shule kuendelea na masomo wakati wazazi wakijipanga kuwanunulia sare hizo.

Bunda. Serikali mkoani Mara imetoa wa mwezi mmoja kwa wanafunzi wasiokuwa na sare za shule kuendelea na masomo wakati wazazi wakijipanga kuwanunulia sare hizo.

Akizungumza mjini hapa leo Jumatatu Januari 17, 2022 wakati wa kupokea madarasa yaliyojengwa na fedha za Uviko-19, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi amesema kuwa lengo la kutoa muda huo ni kutoa fursa kwa kila mwanafunzi apate fursa ya kusoma.

"Hatutaki mtoto yeyeote aliyefaulu apoteze hata siku moja kisa tu hana sare za shule, natoa muda wa mwezi mmoja watoto ambao hawana sare wasome wakati wazazi wakifanya utaratibu" amesema Hapi

Amesema kuwa mradi wa fedha za Uviko-19 katika sekta ya elimu ulilenga kuwapa fursa watoto wote waliofaulu mtihani wa darasa la saba mwaka jana kupata nafasi ya kusoma kwa pamoja hivyo serikali ya mkoa haipo tayari kuona watoto hao wanakosa fursa hiyo kwa kutokuwa na sare.

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Joshua Nassari amesema fedha za Uviko-19 zimejenga madarasa 59 na ofisi 30 za walimu katika wilaya hiyo ambayo yataondoa tatizo la upungufu wa madarasa na ofisi za walimu

"Tumejenga madarasa 59 kwa shule 15 za sekondari na shule shikizi tatu na ofisi 30 ambapo hizi ofisi zitatumiwa na walimu zaidi ya 300” amesema

Kuhusu michango mashuleni, RC Hapi amewaonya walimu wakuu wa shule za kuacha mara moja tabia ya kutumia michango kama kigezo cha kusajili mwanafunzi shuleni.